POLISI SHINYANGA WAONYA WAHALIFU SIKUKUU YA PASAKA…RPC ATAKA WANANCHI KUSHEREHEKEA MAJUMBANI KUKABILIANA NA CORONAKamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akizungumza na waandishi wa habari Aprili 9,2020 - Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba akizungumza na waandishi wa habari Aprili 9,2020 - Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog 
Katika Kusheherekea Sikukuu ya Pasaka Aprili 12,2020, Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba amesema ni vyema wananchi wakakaa nyumbani ili kujiepusha na mikusanyiko isiyo na ulazima ambayo inaweza kusababisha kusambaa kwa Virusi vya Corona ‘Covid 19’. 

Kamanda Magiligimba ametoa rai hiyo leo Alhamis Aprili 9,2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Kipindi cha Sikukuu ya Pasaka kwa ajili ya kuwashirikisha wananchi kuhusu mambo mbalimbali ya ulinzi na usalama huku wito wake ukiwa ni kuwataka wananchi kusherekea kwa amani na utulivu mkubwa. 

“Kutokana na Ugonjwa wa Corona ni vyema wananchi wakasherehekea Sikukuu ya Pasaka Aprili 12,2020 majumbani mwao na waendelee kunawa mikono kwa sabuni na kutumia Sanitizer ili kukabiliana na ugonjwa huu”,amesema Kamanda. 

Katika hatua nyingine amesema Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanasherehekea kwa amani na utulivu bila kujihusisha na vitendo vya uhalifu ama vitendo vingine vyenye viashiri vyovyote vya uvunjivu wa sheria akibainisha kuwa ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya ibada. 

“Nawatahadharisha watumiaji wote wa barabara kuwa makini kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani,ikiwa ni pamoja na madereva kutoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi,kuepuka kuendesha vyombo hivyo wakiwa wametumia vilevi. Jeshi la polisi halitawajibika kumuonea mtu huruma ama upendeleo mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha sheria”,amesema Kamanda Magiligimba. 

Aidha amewaasa wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuendelea kuwa makini zaidi na uangalizi wa watoto wao,watoto wa majirani na watoto wa jamii kwa ujumla waepuke kuwaacha watembee peke yao au kuzurura barabarani na maeneo mengine ili kuepuka ajali na maafa ama matukio yanayoweza kujitokeza na kusababisha madhara kwa watoto. 

“Napenda pia kuwakumbusha wananchi watakaolazimika kutoka katika makazi yao kwenda katika ibada wahakikishe kuwa hawaziachi nyumba/makazi yao wazi pasipo uangalizi ili kama ni lazima kufanya hivyo ni vyema waone umuhimu wa kutoa taarifa kwa majirani zao ili kutekeleza kikamilifu dhana ya Ulinzi Jirani”,ameongeza. 

Amewataka wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mapema pale watakapowatilia mashaka watu wasiowafahamu ama wanaowafahamu kuwa ni wahalifu pindi watakapobaini katika maeneo yao ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo. 

“Nawasisitiza wananchi kuchukua tahadhari kwa kushirikiana na Jeshi la polisi ili kuhakikisha kuwa vitendo vyote vya uhalifu na wahalifu katika maeneo mbalimbali vinadhibitiwa mapema iwezekanavyo iwapo vitajitokeza kwani uzoefu unaonyesha kwamba baadhi ya watu hutumia kipindi cha Sikukuu kufanya matukio ya uhalifu”,amefafanua Kamanda Magiligimba. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post