NAIBU WAZIRI WA ARDHI DR ANGELINA MABULA ATAKA MALIPO YA KODI YA PANGO LA ARDHI KWA MITANDAO YA SIMU KUEPUKA CORONA

Na Munir Shemweta, WANMM SIMIYU

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka wamiliki wa ardhi wanaotaka kilipia kodi ya pango la ardhi kufanya hivyo kupitia mitandao ya simu za viganjani ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia maambukizi ya virusi vya Corona.

Dkt Mabula alitoa tahadhari hiyo juzi wilayani Bariadi mkoani Simiyu alipozungumza na Wakurugenzi na Watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu akiwa katika ziara ya kuangalia utendaji kazi wa sekta hiyo sambamba na kufautilia maagizo aliyoyatoa kuhusiaa na sekta ya ardhi.

Alisema, ni vizuri katika kipindi hiki ambacho kuna maambulizi ya virusi vya Corona wamiliki wa ardhi wakachukua tahadhari ya kutokwenda ofisi za ardhi kulipia kodi ya pango la ardhi na badala yake wafanye malipo kwa kutumia mitandao ya simu.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, malipo ya kodi ya pango la ardhi yanaweza kufanyika kwa kutumia mitandao yote ya simu za viganjani  pamoja na kutembelea tovuti ya Wizara.

‘’Katika kipindi hiki ambacho kuna maambukizi ya virusi vya Corona wadaiwa pamoja na wale wanaotaka kilipia kodi ya pango la ardhi wakafanya hivyo kupitia mitandao ya simu pamoka na kutembelea tovuti ya Wizara ili kuepuka misongamano inayoweza kuchangia maambukizi’’ alisema Dkt Mabula

Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya Pango la Ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu, Dkt Mabula ameoneshwa kutoridhishwa na kasi ya ukusanyaji kodi ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Simiyu pamoja na mkoa huo kusifika katika masuala ya uwekezaji.

‘’ Mkoa wa Simiyu mapato yatokanayo na kadi ya pango la ardhi yako chini sana, lengo la makusanyo kwa mkoa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 ni kukusanya bilioni 10 lakini kiasi mlichokusanya hadi sasa ni milioni 190 tu sawa na asilimia 9.1, inaonesha hamjawa makini kufuatilia madeni’’ alisema Dkt Mabula

Aidha, Naibu Waziri Mabula alisema hata malengo ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi yaliyowekwa katika baadhi ya halmashauri hayaendani na hali halisi na kutolea mfano wa halmashauri ya Busega kuwa na lengo la kukusanya milioni 30 wakati  inadai  milioni 343 kutoka kwa wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi.

Kaimu Mkuu wa mkoa wa Simiyu ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alimuhakikishia Naibu Waziri wa Ardhi,  halmashauri za mkoa huo zitaanza kuwafuatilia wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi  sambamba na kuhakikisha viwanja vinaingizwa katika mfumo na kuwahamaisha wananchi kuchukua hati za ardhi ili kuongeza kasi ya makusanyo ya kodi ya ardhi.

Kiswaga alipongeza maboresho mbalimbali yanayofanywa na wizara ya ardhi katika masuala ya utoaji huduma hizo na kutolea mfano uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa kuwa ni moja ya mambo yatakayoleta ufanisi katika sekta ya ardhi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post