TANZANIA YAFUTA SAFARI ZOTE ZA NDEGE ZA ABIRIA ZA KIMATAIFA KUKABILIANA NA CORONA



Mamlaka nchini Tanzania zimetangaza marufuku ya ndege za abiria kutua nchini humo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo (TCAA) ndege za abiria pekee ndizo ambazo zitaruhusiwa kutua.

Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dkt Hassan Abbas ameandika kupitia mtandao wake wa Twitter kuwa: "Hii ni hatua nyingine ya kupambana na ugonjwa wa Covid-19."

Taifa hilo la Afrika Mashariki mpaka sasa limesharipoti wagonjwa 32 wa virusi vya corona, vifo vitatu na wagonjwa watano kupona.

Maeneo ambayo ugonjwa huo umeripotiwa nchini Tanzania ni Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha na Mwanza.

Marufuku ya usafiri wa anga inasemaje

Kwa mujibu wa tangazo la TCAA, kutokana na mlipuko wa Covid-19 kuanzia tarehe 11 Aprili, masharti yafuatayo yamewekwa: "Ndege zote za kimataifa za abiria ambazo zilikuwa na ratiba ya kutua na hata ambazo hazikuwa na ratiba zinapigwa marufuku kutua."

Kwa upande wa ndege za mizigo zitaendelea kuruhusiwa isipokuwa, "Rubani na wahudumu wa ndege hizo watatakiwa kukaa kwenye karantini katika maeneo yaliyotengwa na serikali kwa gharama zao binafsi," inaeleza tangazo hilo.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post