CAG ABAINI LITA ZA MAFUTA YA PETROL BILIONI 1.4 ZILIINGIZWA NCHINI BILA KUTHIBITISHWA

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Ripoti ya mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali[CAG]katika ukaguzi wake imebaini lita za bidhaa ya petrol bilioni 1.4 kuingizwa nchini bila kuthibitishwa.

Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali[CAG]Charles Kichere amesema katika kupitia ripoti ya utendaji kwa bidhaa za Petroli  zilizoingizwa nchini kwa kipindi kati ya mwaka  wa fedha  2015/2016 na 2018/2019  alibaini lita zipatazo bilioni 9.9 za bidhaa za petrol  ziliingizwa nchini  lakini bidhaa za petrol zilizothibitishwa nchini kwa matumizi ya ndani ni zilikuwa lita bilioni 8.5  na kuwa na tofauti ya lita bilioni 1.4 kati ya bidhaa za petrol  zilizothibitishwa na bidhaa  za petrol zote  zilizoingia nchini kwa matumizi ya ndani.

Bw.Kichere amebainisha tofauti iliyoonekana inaashiria udhaifu katika ufuatiliaji wa bidhaa za petroli zilizoingia nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani  ambapo inaweza kusababisha upotevu wa mapato.

Aidha,Bw.Kichere amesema kati ya mashirika 148 aliyoyakagua  alibaini uwepo wa mashirika 34 yenye wadaiwa sugu yanayofikia kiasi cha Tsh.bilioni 224.69  na  madeni yaliyo mengi yanahusiana na mauzo ya huduma mbalimbali kwa wateja .

Pia mdhibiti na mkaguzi wa hesabu kuu za serikali [CAG] Bw.Kichere amebaini kuwa shirika la Mawasiliano TTCL limekuwa likijiendesha kwa hasara ambapo lilikuwa likitoza bei rahisi kwenye vifurushi inavyouza kwa wateja wake  kuliko bei ambayo inalipa kwa mujibu wa mkataba hali iliyosababisha TTCL kupata hasara ya Tsh.Bilioni 1.11.

Bw.Kichere amebainisha kuwa TTCL imekuwa ikinunua kifurushi cha wiki kutoka kampuni ya MIC  1GB kwa Tsh.2,500 na kuuza kwa wateja wake Tsh.1,500  na kupata hasara ya Tsh.1000  ambapo kwa mwezi  imekuwa ikinunua 20GB  kwa Tsh.50,000 na kuuza  kwa Tsh.40,000 hivyo TTCL kupata hasara ya Tsh.10,000  kwa Mwezi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527