WENYE VIRUSI VYA CORONA NCHINI KENYA WAFIKA 15


Waziri wa Afya wa Kenya Mutahi Kagwe ametangaza kuwa, watu wengine wanane wamethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Corona nchini humo. Ongezeko hilo sasa linafikisha idadi ya watu 15 walioambukizwa virusi hivyo hatari nchini Kenya.


Kwa mujibu wa Waziri Mutahi Kagwe, walioambukizwa ni Wakenya watano na raia watatu wa kigeni walio na umri wa kati ya miaka 20 hadi 57.

Aidha amebainisha kuwa, Wanane hao waliingia nchini kupitia uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta kati ya Machi 4 na 17.

Serikali kwa sasa inafanya juhudi ya kuwatafuta watu 363 walioambatana nao ili kudhibiti maambukizi.

''Inasikitisha kwamba baadhi ya Wakenya wanapuuza maagizo tuliyoweka kukabiliana na ugonjwa huu'' alisema Waziri Kagwe.

Akizungumza na vyombo vya habari Waziri wa Afya wa Kenya amesisitiza umuhimu wa Wakenya kuzingatia hatua zilizowekwa ili kuepusha maafa.

''Huu ugonjwa sio mzaha'' aliongeza kusema. Kenya inasisitiza kuwa wiki mbili zijazo zitakuwa hatari zaidi endapo hali ya maambukizi haitadhibitiwa.

Hatua za dharura zilizochukuliwa kuanzia usiku wa jana  Jumapili, baa zote zitafungwa na wenye hoteli wataruhusiwa kuuza chakula cha kubeba na kwenda kula nyumbani.

Ibada za Kanisa na Swala za pamoja Misikitini zimesitishwa huku mazishi yakiruhusiwa kuhudhuriwa na familia ya marehemu pekee. Sherehe za harusi pia zimepigwa marufuku.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post