WAZIRI MKUU: MAENEO YA SHULE YATUMIKE KWA SHUGHULI ZA KITAALUMA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku shughuli zisizohusiana na taaluma kama ujenzi wa viwanda katika maeneo ya shule ili kutoa fursa kwa wanafunzi kuwa kwenye mazingira mazuri ya kujifunzia.

“Sheria inakataza kuweka matumizi yoyote yasiyokuwa ya kitaaluma katika maeneo ya shule kwani yanasababisha kelele hivyo wanafunzi kushindwa kusoma vizuri.”

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni(Jumanne, Machi 3, 2020) baada ya kupokea malalamiko ya wazazi kuhusu eneo la shule ya msingi Mshikamano iliyoko Halmashauri ya Mji Handeni kuuzwa kwa mfanyabiashara ambaye amefungua karakana ya kutengeneza magari.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu aliuangiza uongozi wa halmashauri hiyo ukazungumze na mfanyabiashara huyo  ili  aondoe karakana katika eneo hilo na kumtafutia eneo mbadala kwa ajili ya kuendesha shughuli zake na eneo hilo libaki kwa ajili ya masuala ya kitaaluma.

Pia, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni upange matumizi bora ya ardhi kwa kuainisha maeneo ya makazi, biashara, viwanda na huduma za kijamii ili kuepuka mji huo kujengwa bila ya mpangilio.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kuwafikisha kwenye vyombo vya dola walimu watakaobainika kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi. “Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike, ukimpa mimba, ukimchumbia au kumuoa adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.”

Akizungumzia kuhusu uwepo wa mabango mengi kwenye mikutano ya hadhara ya viongozi wa Kitaifa, Waziri Mkuu alisema kunadhihirisha wazi kwamba watendaji wa Halmashauri hawawatembelei wananchi katika maeneo yao na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.

“Watendaji hamuendi kuwatembelea wananchi na kusikiliza matatizo yao, haiwezekani wawe wanawasubiri viongozi wa juu na kuwasilisha kero zao, sasa jipangeni haya mabango yote mtakuja kuyajibu kwa sababu hoja zote ni za ngazi ya halmashauri,” alisema.

Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imeelekeza nguvu kubwa katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao, hivyo itasimamia kuhakikisha kila mtumishi anawajibika kwa kiwango kinachostahili.

“Serikali hii haimlindi mfanyakazi ambaye ni mbadhilifu, mwizi na asiyefanya kazi kwa weledi au anayebagua wananchi eti kwa uwezo wake wa kifedha au rangi au dini yake au chama chake. Hivi vitu havipo katika Serikali kila mwananchi aliyeko Nzega anatakiwa kuhudumiwa,”alisisitiza

 (mwisho)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post