WABUNGE WAUNGA MKONO ZUIO LA SERIKALI UAGIZAJI VIFAA VYA UMEME NJE YA NCHI


Veronica Simba – Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imesema inaendelea kuunga mkono zuio la serikali kwa wakandarasi wa miradi mbalimbali ya umeme nchini kuagiza vifaa husika nje ya nchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Machi 14 mwaka huu, baada ya Kamati hiyo kufanya ziara katika viwanda vya Europe Inc. Industries Ltd (Tropical) na Kilimanjaro Cables (T) Ltd (Africab), vinavyozalisha nyaya za umeme na mashine umba (transfoma), Mwenyekiti wa Kamati husika, Dunstan Kitandula alisema uamuzi huo ni mzuri na unapaswa kuungwa mkono.

“Baada ya kutembelea viwanda hivi, tumejiridhisha pasipo shaka kuwa uwezo wake wa uzalishaji unatosheleza mahitaji ya ndani hivyo hakuna sababu ya kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi,” alisema Kitandula.

Akieleza zaidi, Mwenyekiti alisema lengo la ziara yao lilikuwa ni kujiridhisha kuhusu uwezo wa uzalishaji wa viwanda husika kutokana na mkanganyiko uliopo kutokana na baadhi ya wakandarasi kulalamika kuwa vifaa vinavyozalishwa ndani ya nchi havitoshelezi mahitaji yao.

Alisema kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kasi ya utekelezaji miradi ya umeme vijijini hairidhishi na wakandarasi husika wanapoulizwa wamekuwa wakijitetea kuwa hali hiyo inasababishwa na zuio la serikali kuagiza vifaa nje ya nchi.

Hata hivyo, Kitandula alisema mara zote Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa viwanda vya ndani vina uwezo mkubwa kiuzalishaji kwani unakidhi mahitaji ya soko la ndani na hata kuwepo ziada.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Kamati, alitoa wito kwa Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuwasaidia wazalishaji wa ndani katika utafutaji masoko ya vifaa husika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

“Ni lazima sasa ninyi Wizara na REA mvichukulie viwanda hivi kama sifa kwa nchi na mvisaidie kupata masoko nje ya nchi ili kuwawezesha wawekezaji hawa wazalendo kuzalisha kwa tija zaidi na kuepuka hasara inayoweza kuwafilisi,” alisisitiza.

Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Serikali katika suala hilo, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, alisema Wizara imeendelea kuwasaidia wawekezaji wa ndani katika utafutaji masoko nje ya nchi akitoa mfano namna serikali ilivyoisaidia kampuni ya Africab ilipotaka kuwekeza nchini Zambia.

“Niwapongeze Africab kwa uthubutu wao ambao umewawezesha kuanzisha kiwanda nchini Zambia. Walipoenda huko mara ya kwanza, tuliwasaidia kuzungumza na Serikali ya nchi hiyo tukawaeleza uwezo wao wa ndani hatua iliyowasaidia kufanikisha lengo lao. Tutaendelea kufanya hivyo kwa kampuni zetu nyingine,” alisema Naibu Waziri.

Kuhusu suala la baadhi ya wakandarasi wanaosemekana kuendelea kuagiza vifaa nje ya nchi, Naibu Waziri alisisitiza kuwa msimamo wa Serikali ni kutoa adhabu kali za kimkataba na kisheria kwa yeyote atakayebainika kama alivyobainisha Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani hivi karibuni.

Kiwanda cha Africab kina uwezo wa kuzalisha (kwa mwaka) nyaya za umeme kilomita 75,000 transfoma 6,500 na insulators 660,000 wakati Kiwanda cha Tropical kikiwa na uwezo wa kuzalisha transfoma 75,000 na nyaya zinazozidi kwa kiasi kikubwa mahitaji ya soko la ndani.

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iko katika ziara jijini Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya Wizara ya Nishati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527