WABUNGE WATATU CHADEMA, MEYA UBUNGO NA WAFUASI WAO WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUFANYA VURUGU GEREZANI


Viongozi na Wafuasi 27 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),  wamefikishwa Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba yakiwemo ya kutoa maneno ya maudhi kwa askari magereza na kuharibu geti la gereza la Segerea.



Hata hivyo ni washtakiwa 15 tu ndio wamesomewa mashtaka yao leo Machi 23,2020. Hivyo upande wa mashtaka umeomba hati ya wito kwa washtakiwa 12 ambao hawakuwepo leo mbele ya mahakama kujibu mashtaka yao ili waweze kuletwa na kusomewa mashtaka yao.


Washtakiwa hao wamepandishwa kizimbani saa nane mchana leo Jumatatu Machi 23, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.


Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali Mwandamizi Renatus Mkude amewataja washtakiwa hao kuwa ni Halima Mdee Mbunge wa Kawe, Ester Bulaya Mbunge wa Bunda Mjini, Jesca Kishoa Mbunge wa viti Maalimu mkoa wa Singida na Boniphace Jacob Meya wa Ubungo na Diwani wa Chadema Patrick Assenga.

Wengine ni, Henry Kilewo, Yohana Kaunya, Mshewa Karua,  Angela Tryphone,  Khadija Mwango, Reginald Masawe , Pendo Raphael, Cesilia Michael, Happy Abdallah, Paulo Makali.

Mkude amedai washtakiwa walitenda makosa hayo Machi 13 mwaka huu katika Gereza la Segerea.

Amedai wshatakiwa hao wanadaiwa walikaidi amri halali ya Sajent John aliyekuwa katika geti la kuingia gerezani, walifanya mkusanyiko usio halali na waliharibu mali.

Inadaiwa kwa pamoja washtakiwa walishirikiana kufanya uharibifu katika geti kuu la kuingia gerezani, geti ni mali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Pia mshtakiwa Mdee, Bulaya na Boniface wanashtakiwa kwa kutumia lugha ya kuuzi kwa Sajenti John.

Washtakiwa walikana mashtaka, wamekubaliwa dhamana kwa masharti ya kuwa na mdhamini mmoja, mwenye barua na kitambulisho na atasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni nne.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527