Na Amiri Kilagalila,Njombe
Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri ameagiza watoa huduma za baa na wamiliki wa maeneo ya starehe kufunga huduma hizo kwa kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19) ili kuepusha maambukizi na kuenea kwa virusi hivyo.
Ruth Msafiri ametoa agizo hilo mapema siku ya leo wakati akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya ndani ya wilaya hiyo (radio za jamii) kwa lengo la kutoa tahadhari,kutoa elimu na hatua ilipofikia wilaya hiyo katika kudhibiti maambukizi ya CORONA.
“Ninawaomba wauzaji lakini pia wamiliki wa maeneo ya starehe,katika kipindi hiki sio kipindi cha kawaida,kila mtu lazima ajikane mwenyewe,watoa huduma za baa na popote wanapouza vileo wahakikishe inapofika saa nne usiku wafunge hizo huduma kwa kipindi hiki,mtu ambaye anakunywa kaingia saa 12 huyu haiwezi kufika saa nne za usiku akazingatia zile taratibu za kutokugusana,kubusiana wala kukumbatiana,kwa hiyo baada ya masaa hayo mimi ninaamini aende nyumbani kwake alichotumia kinamtosha”alisema Ruth Msafiri
Vile vile mkuu wa wilaya ametoa onyo kwa wafanyabiara wanaoongeza gharama ya vifaa ikiwemo ndoo na vifaa vingine vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID -19 kwa kipindi hiki.
“Nitoe onyo kuna watu wameongeza bei ya ndoo,koki,sanitizer na vile vyote wananvyojua watu wanavikimbilia,jamani huu sio utu,ninaomba tufanye biashara kwa utu na tutengeneze faida kwa njia halali,vyombo vyangu vya uchunguzi vinaendelea kufanya kazi na wote tutakao wabaini tutachukua hatua za kisheria”alisema tena Msafiri
Kwa upande wake mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Njombe Yesaya Mwasubila ametoa wito kwa wananchi wa halmashauri hiyo kufuata na kuzingatia kanuni za usafi na maelekezo ya wataalamu pamoja na serikali ili kujikinga na maambukizi dhidi ya COVID-19 .
“Zipo dalili nyingi za maambukizi ya CORONA ikiwemo kukohoa na dalili vyingine nyingi za kuhisiwa kwa ugonjwa huu lakini nisisitize tu ni lazima mgonjwa awe na historia ya kusafiri kwenda nje ya nchi au anarudi kutoka nchi ambazo zina CORONA lakini pia amekutana na watu ambao wanatoka nchi zenye Corona na tusipozingatia haya tutajikuta tunazusha na kulundika wagonjwa wasio sahihi katika sehemu zilizotengwa,na mpaka sasa katika halmashauri yetu hakuna mgonjwa yoyote wa Corona”alisema Mwasubila.
Halmashauri ya wilaya ya Njombe imeendelea na kutoa elimu madukani,makanisani,stendi,maofisini na hata majumbani dhidi ya maambukizi ya COVID-19 huku ikihamasisha kuwepo kwa vifaa vya kuna mikono na maji safi katika maeneo ya maduka.
Aidha bado katika nchi ya Tanzania kutokana na taarifa iliyotolewa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli kuna wagonjwa wa maambukizi ya virusi vya CIVID-19 wapatao 12.