VIGOGO 6 HALOTEL KORTINI KWA UTAKATISHAJI FEDHA


Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel Son Nguyen (46), na vigogo wengine watano wa Viettel Tanzania wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka 10 yakiwemo ya kuisababishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya zaidi ya Sh bilioni 78.


Washtakiwa wengine ni Nguyen Minh (40) na Vu Tiep Mameneja wa Halotel, Ha Than (39) Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Halotel, Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni hiyo, Nguyen Cong na Kampuni ya Viattel.

Katika hati ya mashtaka iliyosomwa jana mahakamani hapo na wakili wa Serikali Mkuu Monica Mbogo  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, imedaiwa kati ya Juni 8, 2017 na Machi 26,2020 huko Mikocheni washtakiwa waliongoza genge la uhalifu ili kujipatia faida.

Katila shtaka la pili ikidaiwa siku na mahali hapo na katika  maeneo mengine ya nchi ya Tanzania washtakiwa kwa  pamoja walitumia masafa ya redio bila kupata kibali kutoka TCRA.

Imeendelea kudaiwa kuwa kati ya Julai 7,2016 na Machi 26, mwaka huu maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Vietnam washtakiwa kwa pamoja walitengeneza mfumo ambao ulitumia huduma za mawasiliano zinazojulikana kama Virtual Private Network (VPN) kinyume na taratibu.

Aidha washitakiwa hao wanadaiwa kukwepa kulipa kodi kwa TCRA kwa kutumia mitambo ya mawasiliano yaliyounganisha Viettel Tanzania na Vietnam  kinyume na sheria na pia wanadaiwa kutumia masafa ya redio bila kupata kibali cha TCRA ambapo waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 75.

Katika shtaka la sita washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Julai 7, 2016 na Machi 26, mwaka huu kwa kutumia mitambo ya VPN waliisababishia TCRA hasara ya Sh bilioni 3.03 huku pia wakidaiwa kutakatisha Sh bilioni 3.03 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya kuongoza genge la uhalifu.

Hata hivyo washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu ambazo kwa kawaida kusikilizwa mahakama Kuu.
 
 Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 9, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post