TANZANIA YAFANYA VIZURI MFUMUKO WA BEI

Na.Mwandishi Wetu-MAELEZO.

Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa mfumuko wa bei wa taifa umezidi kuimarika kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2020 baada ya kubaki palepale kwenye asilimia 3.7 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioshia Januari 2020.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Bi.Ruth Minja alisema kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioushia mwezi Februari, 2020 imebaki kuwa sawa na kasi ya iliyokuwepo mwezi Januari, 2020.

“Hali hii ya mfumuko wa bei kubaki kuwa sawa kama ilivyokuwa mwezi Januari imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Februari 2020”, alisema  Bi. Ruth Minja.

Aidha ameongeza  kuwa kuna baadhi ya bidhaa za vyakula kama nyama ambayo iliongezeka kwa asilimia 1.6, samaki 6.1, mafuta ya kupikia 2.8, maharage 9.3 na viazi vitamu 4.2. Ongezeko la bei ambalo limekuwepo kwa Februari 2020 ni sawa na ongezeko hilo Februari 2019

Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilipungua bei kwa mwezi Februari, 2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2019 kama vile jiko la gesi ya  kupikia lilipungua kwa asilimia 1.6, viatu vya watoto asilimia 1.0, mafuta ya nywele za  wanawake asilimia 2.5 na  gharama za huduma za starehe asilimia 1.0.

Minja alibainisha kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioisha mwezi Februari, 2020 umeongezeka hadi asilimia 5.9 kutoka asilimia 5.7 kwa mwaka ulioishia Januari 2020.

Aliitaja Tanzania katika Nchi za  Afrika Mashariki kuwa imeendelea kuwa vizuri kwenye mfumuko wa bei kwa asilimia 3.7 ikilinganishwa na Kenya asilimia 6.37 kutoka asilimia 5.78, wakati Uganda mfumuko wa bei umebakia pale pale 3.4 kwa mwaka ulioishia Januari 2020.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post