RC TABORA AWATAKA WANANCHI KUENDELEA KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA CORONA


SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imewataka wananchi kutopuuza maagizo na maelekezo ya Rais Dokta John Pombe Magufuli kuhusu kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa homa ya mafua makali unaosababishwa na kirusi kipya aina ya Corona.

Kauli hiyo imetolewa na na Mkuu wa mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kwenye mkutano maalumu wa aliouitisha kujadili mikakati ya kupambana na jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Corona.

Aliwataka wananchi wote mkoani humo kuungana pamoja katika utekelezaji wa mapambano hayo na kuchukua tahadhari ya juu dhidi ya ugonjwa huo.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa alivitaka vyombo vya habari kutotangaza habari ambazo hazijathibitishwa kwani kufanya hivyo kutawatia hofu wananchi.

Mwanri alisema kuwa kazi ya vyombo vya habari ni kuchukua taarifa ambazo zitasaidia kuelimisha umma juu  kuchukua tahadhari ili wasiweze kuambukizwa ama kuambukiza wenzao.

Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu aliwaasa wananchi kutekeleza maelekezo ya yote wanayoambiwa na wataalamu wa afya kwani ndiyo moja ya kinga ya maambukizi ya magonjwa.

Alisema kuwa suala la kinga ni muhimu sana kwani hadi hivi sasa kirusi kinachoambukiza ugonjwa wa Korona hakijapata tiba.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora Honoratha Rutatinisibwa alisema kuwa wanachi wanapaswa kuzingatia kanuni za afya  na usafi kwa kuwa ndio hatua muhimu  ya kujikinga na corana.

Alitoa wito kwa wananchi na taasisi zote zinazotoa huduma za kijamii kuchukua tahadhari ya kulinda wateja wao ili wasipatwe na maambukizi ya Corona .

Kikao hicho maalumu kimehudhuriwa na Wakuu wa wilaya zote, wananchi, watendaji, wataalamu wa afya , viongozi mbali mbali wa taasisi za dini na mashirika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527