MBOWE ATANGAZA MIKUTANO YA HADHARA NCHI NZIMA


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa kuanzia Aprili 4, 2020, chama hicho kitaanza rasmi kufanya mikutano ya hadhara yenye malengo mawili kudai tume huru na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu. 


Akizungumza na wana habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema lengo pia ni kufanya maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka huu.

Aidha, aliwatangazia viongozi wote wa Chadema katika mikoa na wilaya kuanza kufanya mikutano hiyo licha ya kupigwa marufuku na serikali tangu mwaka 2016 na kwamba hawatahitaji kibali kufanya mikutano hio kwa kile alichodai ni haki yao ya kikatiba.

“Kuanzia Aprili 4, mwaka huu hatutasubiri kibali cha mtu yeyote tutaanza mikutano nchi nzima na kwa kauli hii na watangazia viongozi wote wa Chadema tuanze kufanya mikutano ya hadhara tukidai vitu viwili tume huru ya uchaguzi na maandalizi ya uchaguzi,” alisema Mbowe.

Alisema hatua yake ya kwenda Mwanza katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara, ambazo mgeni rasmi alikuwa Rais John Magufuli, lengo lake lilikuwa kufanyika kwa maridhiano ya kitaifa kati ya vyama na wadau wengine wa siasa, na ndio sababu ya kumwandikia barua ya kuomba kukutana nae, lakini ameshangazwa na kutokujibiwa kwa barua yao hadi sasa.

Kwa mujibu wa Mbowe, kuomba maridhiano kati ya wadau wa siasa na Serikali sio dalili ya uoga bali ni kutaka amani katika nchi.

Aidha, Mwenyekiti huyo alilaani kitendo cha kupigwa na askari Magereza kwa wabunge wanawake wa Chadema ambao ni Mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya walipokwenda kumfuata magereza Ijumaa alipoachiwa, na kwamba kilichofanywa na askari Magereza ni kinyume cha sheria za nchi.

“Mimi nikiwa jela kule nikiwa shambani zimepigwa risasi zaidi ya 13 za moto wanapambana na Mdee, Bulaya na Jesca Kishoa hawa ni wanamama hata katika sheria za Magereza wanaoruhusiwa kushughulika na wanawake ni wanawake tu,” alisema Mbowe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527