RC OLE SENDEKA AWAPA MWEZI MMOJA VIONGOZI KUWATAFUTA WANAFUNZI 708

Na Amiri Kilagalila,Njombe

Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Olesendeka ametoa muda wa mwezi mmoja kwa watendaji,maafisa elimu kata pamoja na viongozi wa mitaa na vijiji kuhakikisha wanawasaka wanafunzi 708 ambao hawajajiunga na masomo ya kidato cha kwanza,vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Sendeka ameonyesha Kukasirishwa na kitendo cha wanafunzi hao 708 waliofaulu kidato cha kwanza na kushindwa kujiunga na masomo.

Ametoa agizo hilo katika kikao cha tathimini ya elimu kilichowakutanisha halmashauri zote za mkoa huo na wadau wa elimu ambapo amesema ni jambo la kushangaza kuona wanafunzi wanagoma kuendelea na masomo wakati serikali imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuboresha miundombinu ya elimu hivyo zoezi la kuwatafuta na kuwapeleka shule wanafunzi ambao hawajajiunga na kidato cha kwanza.

"Nichukue nafasi hii kuwaelekeza wakuu wangu wa wilaya,wakurugenzi watoto wote ambao hawajaripoti kidato cha kwanza,natoa mwezi mmoja kutoka leo,yeyote ambaye atakuwa hajaripoti baada ya hapo watendaji wa kata husika,maafisa elimu,viongozi wa vijiji husika wachukulieni hatua,simamieni ninyi wenyewe na maafisa elimu wenu"alisema Ole Sendeka

Akiweka bayana kuhusu idadi ya wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza, walioripoti na ambao hawajaripoti tangu januari 6 shule zilipofungua ,afisa elimu mkoa wa Njombe Gift Kyando anasema takribani wafunzi 15,711 walifauru lakini asilimia 84.7 pekee ndiyo walioripoti shule na kuitaja wilaya ya Ludewa kuwa na wanafunzi 200 ambao hawajaripoti.

"Kwanza lengo kubwa kwenye mkutano huu ilikuwa ni kuangalia wapi tumetoka na tukaolekea pamoja na mstakabali mzima wa elimu,hali ya kuripoti wananfunzi katika shule zetu waliomaliza mwaka 2019 na kujiunga kidato cha kwanza 2020 si mbaya sana lakini bado kuna wanafunzi ambao hawajaripoti na mpaka sasa ambao hawajaripoti ni 708"alisema Gift Kyando

Nao baadhi ya wadau wa elimu wakitoa mapendekezo ya kuboresha sekta ya elimu akiwemo Flaten Kwahison, Ewdin Mwanzinga na Joram Hongoli mbunge wa Lupembe wanasema ili mkoa uweze kupiga hatua inapaswa kuboresha mazingira ya kupokea na kutoa elimu ,nidhamu na umoja ambayo utekelezaji wake utafanyika kimkakati wa mda mfupi na mrefu.

Katika kikao hicho tuzo za fedha na vyeti zimetolewa kwa halmashauri na shule ambazo zimefanya vizuri kitaaluma. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post