HALI YA DHARURA YATANGAZWA MAREKANI BAADA YA VIRUSI VYA CORONA KUUA MTU MMOJA


Gavana wa jimbo la Washington nchini Marekani ametangaza hali ya dharura ya kiafya baada ya mtu mmoja kuaga dunia kutokana na virusi vya Corona katika jimbo hilo, hii ikiwa ni kesi ya kwanza virusi hivyo kuua nchini Marekani.

Gavana Jay Inslee ameziagiza idara zote za serikali ya jimbo hilo kutumia rasilimali zote kupambana na mripuko na maambukizi ya Corona baada ya kifo hicho kuripotiwa jimboni hapo.

Maafisa wa majimbo ya Marekani ya California, Oregon na Washington wana wasiwasi mkubwa wa kuenea kwa virusi hivyo baada ya kesi nyingi kuthibitishwa miongoni mwa watu wa jamii za West Coast nchini humo.

Rais Donald Trump ambaye siku ya Ijumaa aliwashambulia viongozi wa chama cha Democratic ambao wametilia shaka uwezo na utayarifu wa serikali yake katika kukabiliana na maambukizi ya virusi hatari vya Corona nchini humo ametaka Wamarekani kutokuwa na hofu baada ya kifo hicho kuripotiwa, akidai kuwa virusi hivyo vitatoweka vyenyewe kimiujiza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527