MKURUGENZI WA WILAYA BABATI AWAONDOA WAFANYABIASHARA MNADANI KUHOFIA CORONA


Na John Walter-Babati
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Hamisi  Malinga amezuia mnada maarufu wa Maole uliokuwa ufanyike leo Machi 18,katika kijiji cha Maweni kata ya Magara mkoani Manyara.



Malinga amesema baada ya agizo lililotolewa na serikali kupitia kwa waziri Mkuu Kasim Majaliwa kwa sasa wanachofanya wao ni utekelezaji wa agizo hilo na kwamba asubuhi ya leo wamesisitiza tangazo hilo kwa wafanyabiashara.

Amewataka wafanyabiashara hao kutii agizo la serikali na kujali Ubinadamu kuliko biashara zao na kusubiri hadi hali ya maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona itulie na kusubiri tangazo lingine la serikali litakapotolewa.

Amesema anatambua fika kuwa mnada huo unaingiza kipato kikubwa kwa Halmashauri ya wilaya ya Babati na mkoa kwa ujumla,lakini afya na maisha ya watu ni muhimu kuliko mapato yanayopatikana.

Mnada huo maarufu uaofanyika kila jumatano, huwakutanisha wafanyabiashara mbalimbali kutoka Mkoa wa Arusha na Manyara .

Jana Machi 17,2020, Serikali ilisitisha mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli nyingine za kijamii na kufungwa  shule zote za awali, msingi na sekondari kwa siku .

Pia Waziri mkuu aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe maeneo yote yaliyobainishwa na kutengwa (vituo vya huduma na ufuatiliaji) kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa endapo watajitokeza katika maeneo yao yanakuwa na mahitaji yote muhimu na yanahudumiwa ipasavyo.

Mpaka sasa serikali imethibitisha kuongezeka kwa wagonjwa wawili wa Corona na kufanya idadi ya walioambukizwa kufika watatu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527