Breaking: WAGONJWA WA CORONA WAFIKIA WATATU TANZANIA ......VYUO VIKUU VYAFUNGWA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa idadi ya wagonjwa wa Virusi vya Corona nchini imeongezeka na kufikia watatu, ambapo mmoja amepatikana Zanzibar ambaye ni raia wa Ujerumani na mwingine Jijini Dar es Salaam ambaye ni raia wa Marekani.

“Tuna ongezeko la wagonjwa wawili ambao wamethibitika kuwa na corona Tanzania. Tuna mgonjwa mmoja kutoka Zanzibar ambaye sampuli zake zililetwa maabara kuu ni Mjerumani (24) amepata maambukizi yupo kwenye uangalizi, lakini pia hapa jijini Dar es Salaam na Mmarekani mwenye miaka 21 naye amegundulika kuwa na virusi vya corona,” amesema Majaliwa.

Aidha Majaliwa amesitisha masomo ya vyuo vikuu na kati na vyuo ambavyo wanafunzi wako likizo wametakiwa kubakia nyumbani ili kukabiliana na Virusi vya Corona.



“Wale wachache ambao wanamalizia mitihani wakimaliza waondoke mara moja ili kuondoa misongamano na vyuo vya kati vya ufundi na ualimu waliotakiwa kufanya mtihani Mei mwaka huu namuagiza Waziri wa Elimu afanye marekebisho ya mihula ya elimu kama ya kidato cha sita”,amesema.

Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea na shughuli za kila siku na taarifa zitazidi kutolewa na shughuli mbalimbali zitaendelea kusitishwa kutokana na hali itakavyokua.

Amesisitiza kutofanya misongamano na mikusanyiko isiyo na umuhimu huku shughuli za masoko na maduka zitaendelea.

“Huduma za usafirishaji zitaendelea lakini wasafirishaji waendelee kuwaelimisha abiria hakuna umuhimu wa kujaza watu wakikaa kwenye viti gari iende.

Serikali imesema inaendelea kuwahifadhi wagonjwa hadi ugonjwa huo utakapoisha na hatua zinaendelea kuchukuliwa katika mipaka na sehemu za uingiaji wageni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527