MAANDALIZI YA KUKABILIANA NA CORONA SONGWE YAFIKIA HATUA NZURI


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameibanisha Kuwa maandalizi ya kukabiliana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa Mkoa wa Songwe yapo vizuri huku akizielekeza Halmashauri za Wilaya kukamilisha baadhi ya mapungufu yaliyopo.

Brig. Jen. Mwangela ameyasema hayo jana akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa mara baada ya kukamilisha ukaguzi wa utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona katika Halmashauri  za Mbozi, Ileje na Halmashauri ya Mji Tunduma.

Amesema watalaamu wa Afya ambao watawahudumia wagonjwa wa Corona endapo watatokea Mkoani Songwe tayari wana mafunzo na Uelewa wa majukumu yao huku Vituo vilivyo teuliwa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na washukiwa vimezingatia maelekezo ya Wizara ya Afya.

Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa amebaini baadhi ya vituo vya kutolea huduma kwa wagonjwa na Washukiwa wa Corona vina mapungufu kadhaa ikiwemo uhaba wa maji, umeme na baadhi ya vifaa tiba na kinga ambapo ameziagiza Halmashauri husika kukamilisha mahitaji hayo haraka sana.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa elimu ya Kujikinga na Virusi vya Corona kwa wasafiri, madereva na wafanyakazi wengine wa Mabasi katika maeneo mbalimbali huku akiwasisitiza kuchukua hatua za tahadhari kwa kunawa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya Lazima.

Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi George Salala amewaagiza wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha hawajazi abiria kuliko uwezo wa gari kwakuwa ni kutengeneza mkusanyiko usio wa lazima huku akisema hatua kali zitachukuliwa kwa watako kaidi.

Kamishna Msaidizi wa Polisi Salala ametoa angalizo kwa abiria pia kutokubali kupanda mabasi au usafiri endapo watakuta umejaa kwani mikusanyiko kama hiyo ni mojawapo ya njia ya kusambaza ugonjwa wa Virusi vya Corona.

Amesema wamiliki wa mabasi wanapaswa kuweka maji ya kunawa yenye dawa katika mabasi yao ili kuwakinga madereva wao na kuwakinga abiria dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwakuwa ili kufanikisha kutosambaa kwa ugonjwa huo inatakiwa jamii yote ishirikiane.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamad Nyembea amesema mpaka sasa maandalizi ya Utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Corona kwa Mkoa wa Songwe yamefikia asilimia 50 huku mapungufu yaliyobainishwa yatakamilishwa ifikapo mwishoni mwa wiki hii.

Dkt Nyembea ameongeza kuwa kufuatia agizo la Serikali la kuwaweka karantini siku 14 watu wote walio toka nchi zenye maambukizi Zaidi ya Virusi vya Corona hadi sasa wamewaweka watu sita karantini waliotumia mpaka wa Tunduma kutokea nchi ya Afrika Kusini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527