SERIKALI YAAGIZA WAKIMBIZI 1000 WALIOTOROKA MAKAMBINI NA KWENDA KUFANYA UHALIFU WAONDOLEWE NA WAFUNGULIWE MASHITAKA

Na Mwandishi Wetu,Kibondo

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameviagiza Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoani Kigoma kuwaondosha na kuwafungulia mashtaka wakimbizi zaidi ya Elfu Moja waliotoroka kutoka katika Kambi mbalimbali za wakimbizi  na kwenda kufanya uhalifu nje ya makambi.

Naibu Waziri Masauni ameyasema hayo leo  wakati akiongea na wakimbizi kutoka nchini Burundi waliohifadhiwa katika Kambi ya Nduta iliyoko wilayani Kibondo, mkoani Kigoma huku ikihifadhi jumla ya wakimbizi na waomba hifadhi 75,055.

“Tanzania na Burundi zimekua zikishirikiana kwa muda mrefu,Tanzania si nchi ya kubembeleza watu waovu na haijawahi kufuga wahalifu , kuna watu zaidi ya Elfu Moja  wamevunja sheria za ukimbizi kwa kutoroka kwenye makambi na kwenda kufanya uhalifu huko nje, sasa naviagiza vyombo vya usalama kuhakikisha wanawaondosha hao watu kwa mujibu wa sheria na itakua fundisho kwa watu wote wenye tabia ya kutoroka makambini na kwenda nje  kufanya uhalifu, ” alisema Masauni

Masauni pia aliwataka wakimbizi hao kuendelea kujiandikisha  kwa hiari ili waweze kurudi nchini kwao Burundi ambako hali ya amani sasa imerejea na tayari pande tatu ikiwemo Serikali ya Tanzania, Serikali ya Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) washatiliana saini mkataba utakaofanikisha zoezi hilo kwa wanaotaka kurejea Burundi

“Serikali ya Burundi imetuthibitishia kurejea kwa amani katika nchi yenu, nendeni mkaijenge na kuitumikia  nchi  yenu, nchi yoyote ili iweze kuendelea  inahitaji  watu na hapa naona kuna vijana wengi tu ambao ndio msingi wa maendeleo wa nchi yoyote ile duniani”aliongeza Masauni

Akizungumza katika Mkutano huo Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kibondo,  Kanali Hosea Ndagala aliwataka wakimbizi hao kufuata sheria za nchi na wao kama Kamati ya Ulinzi na Usalama watahakikisha kila atakaethibitika kufanya uhalifu sheria itachukua mkondo wake ikiwemo kufutiwa ukimbizi na kufunguliwa mashtaka.

“Hatutoruhusu mtu yoyote kuingiza vitu visivyoruhusiwa katika makambi ambavyo vinaweza kuhatarisha usalama katika makambi yenu na tunaomba mkiona kitu chochote kisicho cha kawaida mtoe taarifa kwa viongozi ili mbakie katika mazingira salama” alisema Kanali Ndagala

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo wakimbizi hao waliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwahifadhi na kuwapa huduma ya ulinzi huku wakiomba kuwahishiwa huduma mbalimbali ikiwemo nguo,chakula na huduma za afya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post