Picha : MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA JASINTA MBONEKO AFANYA ZIARA KUKAGUA MIRADI YA MAJIMkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika eneo la Uzogole, Lubaga pamoja na Masengwa, miradi ambayo itawaondelea changamoto wananchi ya ukosefu wa maji safi na salama.

Mboneko amefanya ziara hiyo leo Machi 19,2020, kwa kukagua utekelezaji wa miradi hiyo ya maji yanayotoka Ziwa Victoria, kwa usimamizi wa Wakala wa Maji Vijjini (RUWASA), kwa kushirikiana  na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA).

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo ya maji, Mboneko amewataka wananchi ambao wanatekelezewa miradi hiyo waitunze miundombinu yake na kutoiharibu, ili idumu kwa muda mrefu pamoja na kuwaondolea adha ya kutumia maji ambayo siyo salama kwa afya zao.

Amesema Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi  kutekeleza miradi ya maji kwa wananchi, hivyo ni vyema miradi hiyo wakaitunza huku akiwataka wasimamizi wa vituo vya kuchotea maji wawepo muda wote ili wananchi wasikose huduma ya maji hata mara moja.

“Leo nimefanya ziara ya kukagua miradi hii ya maji ambayo inatekelezwa kwa fedha za Serikali katika eneo la Uzogole, Lubaga, pamoja na Masengwa ili kuona inaendeleaje na wananchi waanze kutumia huduma hii ya maji safi na salama, maji kutoka Ziwa Victoria,” amesema Mboneko.

“Na kwenye vituo vya kuchotea maji mfano hapa Lubaga ambapo mradi umeshakamilika na kuanza kutoa maji, wasimamizi wa kituo hicho wauze maji kwa kufuata bei elekezi ya Serikali Shilingi 25 kwa ndoo moja, na siyo kuzidisha na uongozi usome mapato na matumizi kwa wananchi,”ameongeza.

Pia amemtaka mkandarasi anayejenga mradi wa maji Masengwa (Emirates Bulder) aongeze kasi ya utandazaji wa mabomba ya maji pamoja na ujenzi wa tenki la maji, ili mradi huo ukamilike haraka na wananchi waanze kutumia maji safi na salama.

Aidha amempongeza mkandarasi huyo kwa kutekeleza agizo la Serikali, la kununua vifaa vya kutekelezea mradi huo wa maji Masengwa kutoka ndani ya nchi jambo ambalo litakuza uchumi wa nchi.

Naye Kaimu Meneja Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Shinyanga  Emmael Mkopi, alisema katika mradi wa maji Uzogole, ulianza Februari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Aprili 15, 2020 kwa gharama ya Shilingi Milioni 150, ambap mradi wa Masengwa ulianza Juni 2018 na utakamilika Aprili 27 mwaka huu na umegharimu Shilingi Bilioni 4.19.


TAZAMA PICHA HAPA CHINI

Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, akifungua maji kwenye mradi wa maji Lubaga ambao umeshakamilika kwa kutekelezwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) leo Alhamis Machi 19,2020 wakati akifanya ziara ya kutembelea miradi ya maji katika wilaya ya Shinyanga .Kushoto ni Meneja Ufundi wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Kushoto ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Flaviana Kifizi, akimuelezea Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko namna mradi wa Maji Lubaga utakavyomsaidia pia mwanamke jinsi ya kubeba ndoo ya maji na kutoinama kuepuka kuumia mgongo.

Mzee Martine Shila mkazi wa Uzogole akiipongeza Serikali pamoja na mkuu huyo wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, kwa kutekeleza mradi huo wa maji safi na salama.

Kushoto ni Meneja ufundi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) Mhandisi Yusuph Katopola, akiingiza namba kwa ajili ya kununua maji kwa mfumo wa Luku kwenye mita ya maji Uzogole, kulia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, akikagua zoezi la uchimbaji mitaro kwa ajili ya kulaza mabomba kwenye mradi wa maji ya Ziwa Victoria eneo la Uzogole.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (katikati), akikagua ubora wa mabomba ambayo yatawekwa kwenye mradi wa maji ya  Ziwa Victoria katika eneo la Uzogole. Kulia Kaimu Meneja Wakala wa Maji  Vijijini (RUWASA) Emmael Mkopi, kushoto ni Meneja ufundi wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akikagua ubora wa mabomba ambayo yanatandazwa kwenye mradi wa maji Masengwa, kulia ni msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Emirates Bulder ya jijini Dar es salaam Said Msangi.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko, akikagua ufukiaji wa mabomba kwenye mradi wa maji Masengwa.

Zoezi la ufukiaji mabomba likiendelea.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (katikati) akiangalia namna mabomba yanavyounganishwa kwenye mradi wa maji Masengwa.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko (kushoto) akiangalia namna mabomba yanavyounganishwa kwenye mradi wa maji Masengwa.

Mabomba ambayo yanatandazwa kwenye mradi wa maji Masengwa.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza na wananchi wa Isela na kuwataka wakulima wa mpunga wakipata fedha wajenge nyumba bora na vyoo bora. Wananchi hao waliomba wapate pia maji ambapo Mkuu huyo wa wilaya aliwaambia kuwa watapata kwa mradi mwingine wa Wafaransa wa kusambaza maji kutoka katika mabomba makubwa.

Awali mkuu wa wilaya ya Shinyanga  Mhe. Jasinta Mboneko akiwa Uzogole,akigawa Jezi ya mpira pamoja na mpira katika timu ya vijana ya Uzogole, kushoto ni Nahodha wa timu hiyo Mussa Juma.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akigawa Jezi za mpira kwa timu ya Veterani ya Uzogole, kushoto ni Nahodha wa timu hiyo Paulo Maige.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiangalia Green house ya zao la nyanya iliyopo katika eneo la Nhelegani Kata ya Kizumbi.

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post