KINACHOENDELEA BAADA YA DARAJA LINALOUNGANISHA MOROGORO NA DODOMA KUSOMBWA NA MAJI

Mamia ya abiria waliokuwa wakitoka na kwenda Mikoa ya Morogoro na Dodoma na maeneo jirani leo Jumatatu Machi 2, 2020 wamekwama kuendelea na safari kutokana na daraja la Kiyegeya lililopo eneo la Gairo kusombwa na maji.

Tukio hilo lilitokea leo Jumatatu Machi 2,2020 saa 9 alasiri na kusababisha waliokuwa katika mabasi na magari binafsi kukwama eneo hilo.

Magari kutoka Morogoro kwenda Dodoma na kutoka Dodoma kwenda Morogoro pamoja na mikoa jirani hadi saa 12 jioni yalikuwa yamekwama eneo hilo.

Baadhi walilazimika kugeuza na kutumia njia mbadala kuendelea na safari.

Mmoja wa abiria aliyekuwa akielekea Dodoma, Lulu Kansary alilieleza Mwananchi kwa njia ya simu kuwa walifika eneo hilo saa 10 jioni lakini walikuta umati mkubwa wa watu na foleni ya magari.

“Ilibidi dereva na abiria tushuke na kwenda moja kwa moja eneo husika kuangalia. Wataalamu wanadai makadirio ni mita kati 15 hadi 20 ya eneo lililosombwa na maji.”


“Kwa sasa tumeamua kugeuza na kurudi Morogoro mjini maana mazingira ni magumu ya kwenda Dodoma kutokana na eneo lile kutopitika. Tukifika Morogoro tutajua nini cha kufanya,” alisema Lulu.

Akizungumzia kukatika kwa daraja hilo mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare amesema mabasi ya abiria na magari madogo yanayotumia Barabara ya Morogoro-Dodoma yanatakiwa kutumia njia mbadala ya Iringa.

Alisema hadi leo saa 12 jioni wataalam mbalimbali wamefika eneo la tukio kwa ajili ya kuanza matengenezo.
Via Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post