Waziri Mkuu Majaliwa Kasema Leo Jumapili Kuwa Watanzania Waliopo Wuhan nchini China Wapo Salama

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema vijana wa Tanzania wapatao 497 wanaosoma katika vyuo mbalimbali vilivyoko kwenye mji wa Wuhan nchini China wote wapo salama.

Kwa sasa Mji wa Wuhan umewekewa zuio hakuna mtu anayeruhusiwa kutoka wala kuingia, lengo likiwa ni kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo. Mlipuko wa virusi vya corona ulianzia katika mji wa Wuhan.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Februari 16, 2020) kwenye Kumbukumbu ya Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam iliyoandaliwa na Nida Textile Mills (T) ltd, na kufanyika katika mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar-es-Salaam. Watu zaidi ya 1,500 wamefariki dunia kutokana na mlipuko wa virusi hivyo.

Waziri Mkuu amesema kutokana na zuio hilo wakazi wote wa mji huo wakiwemo vijana wa Kitanzania wanapata huduma mbalimbali kupitia njia ya mtandao ukiwemo ununuzi wa bidhaa mbalimbali.

“…Hakuna usafiri hata wa umma unaofanya shughuli za kusafirisha watu katika mji wa Wuhan kila mmoja anaetakiwa abakie katika makazi yake na kwamba Serikali ya China na uongozi wa vyuo unawatunza wanafunzi wote wakiwemo na Watanzania.”

Waziri Mkuu amesema kwamba kwa sasa Wachina wameimarisha utoaji huduma kwa njia ya mtandao hata kama mtu anataka kununua kitu ananunua kwa njia ya mtandao. “Kama kijana ameishiwa basi atumiwe fedha kwa njia ya mtandao ili aweze kujikimu wakati huu wa zuio.”

Waziri Mkuu amesema jambo la muhimu kwa sasa ni usalama wao na kujali maelekezo yaliyotolewa na Serikali ya China juu ya usalama wao pamoja na wananchi wengine walioko katika eneo hilo.

Amesema Serikali imeweka mitambo ya kupima watu katika maeneo yote ya mipaka na kwamba inawataka wananchi washirikiane nayo katika kuhakikisha watu wote wanaoingia nchini wanapita kwenye njia sahihi.

Pia, Waziri Mkuu amerua kuwataka Watanzania waendelee kuwa watulivu na kuitegemea Serikali katika kupata taarifa za mara kwa mara kuhusu masuala mbalimbali zikiwemo na ya mlipuko wa virusi hivyo.

(MWISHO)
IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments