Watumishi Wizara Ya Mambo ya Nje Watakiwa Kuchapa Kazi Kwa Bidii na Ushirikiano

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Katibu Mkuu mpya, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge. 
 
Mhe. Prof. Kabudi ametoa rai hiyo jana jijini Dodoma wakati wa kikao na Watumishi wa Wizara ambapo pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilitoo fursa ya kutakiana heri ya mwaka mpya 2020 na kumkaribisha Wizarani Katibu Mkuu Mpya, Balozi Kanali Ibuge  kilichofanyika 
 
Aidha, mhe. Prof. Kabudi aliwaeleza watumishi hao kuwa, mwanzo wa mwaka ni kipindi kizuri cha kujipanga na kuweka mikakati ya namna bora ya kutekeleza majukumu  kwa ajili ya maendeleo ya Taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Joseph Pombe Magufuli.
 
Kadhalika amewataka kufanya kazi kwa bidii, kujitambua na kujenga umoja  na ushirikiano katika kutekeleza majukumu hayo kikamilifu.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge ameahidi ushirikiano kwa watumishi wa Wizara na kuwakumbusha kuwa kila mmoja ana wajibu mkubwa wa kuchangia maslahi mapana ya Taifa ili mradi kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa kuendelea kujituma, kuwa tayari kurekebishwa, kuwa watiifu na kuwa tayari kupokea maelekezo.
 
"Watumishi wenzangu, kila mmoja hapa ana mchango mkubwa kwa maslahi ya Taifa letu. Ninasisitiza kuwa mwendelee kujituma, kufanya kazi kwa weledi, kuwa watiifu, kuwa tayari kurekebishwa na kuwa tayari kupokea maelekezo. Binafsi nitaendelea kutoa usikivu kwenu kama ilivyokuwa kwa watangulizi wangu" alisema Balozi Ibuge. 
 
Kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili Wizara, Balozi Kanali Ibuge amewataka Watumishi wote kushirikiana kuzitatua kwani hakuna changamoto ya kudumu endapo Watumishi wote watakuwa kitu kimoja.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post