UNESCO YATAMBUA KISWAHILI KAMA LUGHA ITAKAYOSAIDIA KUKUZA UTANGAMANO BARANI AFRIKA


Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeitambua Lugha ya Kiswahili kama lugha itakayosaidia kukuza utangamano Barani Afrika wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Lugha Mama yenye kaulimbiu “Lugha Bila Mipaka” iliyofanyika jijini Paris, Ufaransa hivi karibuni.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kwa kushirikiana na UNESCO uliandaa mjadala kuhusu "Fursa na Changamoto za Kukitambua Kiswahili kama Lugha rasmi ya Bara la Afrika kwa ajili ya kukuza Utangamano".

Akizungumza wakati wa Mjadala huo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Mhe. Samwel Shelukindo pamoja na mambo mengine, alieleza hatua iliyochukuliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha zitakazotumika katika Jumuiya hiyo.

Aidha, Mhe. Balozi Shelukindo alizipongeza nchi za Afrika Kusini na Namibia kwa kuwa nchi za kwanza Kusini mwa Afrika zilizoamua kuanzisha ufundishwaji wa lugha ya Kiswahili katika shule mbalimbali. Mjadala huo uliwashirikisha Wataalam mbalimbali akiwemo Prof. Aldin Mutembei kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,

Kufanyika kwa mjadala huo katika UNESCO ni moja ya juhudi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa za kukifanya Kiswahili kuwa moja ya lugha zitakazotumika katika UNESCO.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527