SIMBA SC YAING’OA KWA MATUTA STAND UNITED CCM KAMBARAGEMABINGWA wa soka Tanzania, Simba SC wamefanikiwa kwenda Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa penalti 3-2 kufuatia sare ya 1-1 na wenyeji, Stand United jioni ya leo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Meddie Kagere alikosa penalti ya pili katika mchezo wa pili mfululizo leo baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa wa Stand United, Murtala Hamad ambao ndio ulifungua ngwe ya matuta leo.

Kagere alikosa penalti pia kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, ingawa Simba SC iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Biashara United naye akifunga bao la pili siku hiyo.
Waliofunga penalti za Simba SC leo ni viungo, Mzambia Clatous Chama, Mkongo Deogratius Kanda na mzawa, Hassan Dilunga, wakati Ibrahim Ajibu shuti lake liligonga mwamba wa juu na kupotelea nje.

Kwa upade wa Stand United penalti zao zilifungwa na Fakhi Juma na Brown Raphael, huku Miraj Saleh akigongesha mwamba, Majid Kimbondile akipiga juu kabisa na Maulid Fadhil akagongesha mwamba wa kulia mpira kwenda nje.

Awali Simba walitangulia kwa bao la mkwaju wa penalti wa Dilunga dakika ya 51, kufuatia beki wa Stand United, Antidius Ishengoma kuunawa mpira kwenye boski, kabla ya wenyeji kusawazisha kupitia kwa Miraj Saleh dakika ya 67.

Stand United ilimaliza pungufu mchezo huo, baada ya mchezaji wake, Abdi Mwite kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 75 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kujiangusha.

Kikosi cha Stand United kilikuwa; Murtala Hamad, Severine Charles, Antidius Ishengoma, Yela Mboma, Majid Kimbondile, Fakhi Juma, Amri Msenda, Abdi Mwete, MIraj Saleh, Maulid Fadhil na Zamogoni Pangapanga/Brown Raphael. 

Simba SC; Benno Kakolanya, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Tairone Santos, Kennedy Juma, Gerson Fraga ‘Viera’, Hassan Dilunga, Sharaf Eldin Shiboub/chama, Meddie Kagere, Ibrahim Ajibu na Shiza Kichuya/kanda. 

Mechi nyingine za 16 Bora leo, Sahare All Stars iliungana na Simba kutinga Robo Fainali baada ya kuwachapa Panama FC 5-2 Jijini Dar es Salaam, Namungo FC nayo ikaichapa 2-1 Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wakati Ndanda SC ikashinda 2-1 dhidi ya Kitayosa FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Hatua ya 16 Bora itakamilishwa kesho kwa mechi nyingine nne, Yanga wakiwakaribisha Gwambina FC Uwanja wa Uhuru, JKT Tanzania na Alliance FC, Dar es Salaam, Kagera Sugar na KMC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na Ihefu FC dhidi ya mabingwa watetezi, Azam FC Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post