SERIKALI YATOA ELIMU KWA WACHIMBAJI WA DHAHABU JUU YA MADHARA YA MATUMIZI YA ZEBAKI ILI KULINDA AFYA ZAO

Na Robert Hokororo, Singida

Wakati Serikali inaendelea kuweka utaratibu wa kupata mbadala wa matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu imeshauri watumie vifaa vinavyowakinga wakati wakifanya shughuli hizo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima wakati akizungumza na wachimbaji wadogo kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Sambaru wilayani Ikungi na Londoni wilayani Manyoni mkoani Singida.

Sima alisema kuwa Serikali inaendelea na kuwapa elimu wachimbaji hao katika maeneo mbalimbali nchini ili waweze kuepuka madhara ya kiafya yanayotokana na kemikali hiyo.

“Tanzania tuliridhia Mkataba wa Minamata mwaka jana unaotaka kupunguza ama kuondoa kabisa matumizi ya zebaki kwa ninyi wachimbaji ili kuwaepusha madhara ya kiafya na kimazingira katika maeneo yenu,” alisema naibu waziri.

Akiwa katika ziara hiyo ambapo alitembela kuona shughuli za uchimbaji na kukagua namna wanavyotunza mazingira, Sima alisema kuwa jukumu la Serikali ni kutoa elimu juu ya madhara ya zebaki ili kulinda afya za wachimbaji wadogo.

 “Niwaahidi tu tutashirikiana na Ofisi ya Madini ili muweze kupata vifaa maalumu vya kujikinga wakati wa kuchenjua badala ya mikono, tutawaletea gloves mvae mikononi na musk wakati tunachoma ili kufunika pua kwani kemikali hii ina madhara kiafya,” alisema.

Aidha, Naibu waziri aliwataka wachimbaji hao kuacha kukata miti wakati wa shughuli za uchimbaji wa dhahabu na badala yake wawe na utamaduni wa kutumia njia mbadala kama ambavyo wanavyoelekezwa na mamlaka zinazohusika.

Aliongeza kuwa jukumu la Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla ni kuhakikisha nchi inakabiliana na changamoto ya mabadilkko ya tabianchi na hivyo kuleta athari.

Alisema tunapoendelea kuchoma na kukata miti ovyo, kulima kholela na kuchimba mashimo ovyo kwa ajili ya madini ni mambo yanayosababisha mvua isije kwa wakati pamoja na jua kuwa kali kuliko kawaida.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527