RPC SHANA AMPA ONYO GODBLESS LEMA KUHUSU SAKATA LA BARABARA ZA NGORONGORO


Jeshi la Polisi mkoani Arusha limemtaka Mbunge Godbless Lema, kutoingilia kazi zake, kwani lazima litayatekeleza maagizo ya Mkuu wa Mkoa huo, aliyetaka kukamatwa kwa waliohusika kusambaza video, zinazoonesha ubovu wa miundombinu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, bila kujali nafasi zao.

Hayo yamebainishwa leo Februari 17, 2020, na Kamanda wa Polisi Mkoani Arusha Jonathan Shana na kusema kuwa Lema aache masuala ya kisiasa na kwamba badala ya yeye kushangaa kuona watu wakikamatwa kwa makosa ya kiuchochezi, bali Jeshi hilo litamshangaa yeye kwa kukosa uzalendo.

“Nimeona Mhe Lema Mbunge wa Arusha Mjini anasema atashangaa kuona watu wakikamatwa kwa Uchochezi, natumia fursa kumtahadharisha akae mbali na suala hili wakati huu ambao Jeshi kabambe lipo kazini kuhakikisha Mkoa unaendelea kuwa Salama na Utalii unashamiri” ilisema taarifa hiyo.


Aidha Kamanda Shana alibainisha umuhimu wa Sekta ya Utalii nchini na kusisitiza kwamba yeyote atakayeonekana kuikwamisha sekta hii atashughulikiwa kama Mhujumu Uchumi.Kamanda Shanna  kupitia taarifa hiyo,alisema kuwa,jeshi la polisi limepokea maelekezo ya Mhe Mrisho Gambo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Arusha na Mwenyekiti kabambe ya usalama mkoa ,ya kuhakikisha wachochezi wote pamoja na wanaochafua taswira nzuri ya nchi yetu wanakamatwa Mara moja nasi tumelipokea agizo hili na tutatekeleza kwa asilimia Mia moja .Alifafanua kuwa,jeshi Hilo litahakikisha linawasaka kila Kona ya mkoa na mahali popote walipo bila kujali nafasi zao walizonazo.“Namshauri mbunge Lema asikariri na asome alama za nyakati maana hii si awamu ya mchezomchezo naamini kwa pamoja tunaweza ,uzalendo wetu Kwanza na siasa baadaye.”alisema Kamanda Shanna.“Utalii unachangia 17.5% ya pato lote la Taifa, Utalii unachangia 25% ya fedha zote za kigeni, Ngorongoro mapato yake ni 143 Billion kwa mwaka, Ngorongoro inatoa gawio la Serikali kiasi cha 23.5 Billion kwa mwaka, Mapato ya Tanapa ni kiasi cha Bilioni 282.42 kwa mwaka,hili ni suala linalohusu uchumi wa nchi yetu kwa hiyo wanasiasa wasilete siasa wala masihara kwenye uchumi wa Nchi” ilisema taarifa hiyo.Kamanda Shana amesisitiza Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linaendelea kufanya upelelezi wa wale wote waliohusika na uhalifu huo na mara watakapobainika watafikishwa katika vyombo vya dola.


Juzi Mkuu wa Mkoa huo Mrisho Gambo, alitoa agizo hilo na kudai kuwa waliosambaza video hiyo wanayo nia ya kuhujumu uchumi wa Taifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post