KIJANA AFARIKI DUNIA KWA KUNYWA POMBE KUPITA KIASI SHINYANGA MJINI



Wananchi wa mtaa wa Dome kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga wakiangalia mwili wa marehemu Nkuba Mawe ambaye amedaiwa kufariki dunia kwa sababu ya kunywa pombe kali kupita kiasi.Picha na Marco Maduhu - Malunde 1 blog
Jeshi polisi likiubeba mwili wa marehemu


Na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Mkazi wa Ukenyenge wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Nkuba Mawe (27) amekutwa amefariki dunia kwenye vibaraza vya maduka katika mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga eneo ambalo alikuwa akiishi kwa sasa kwa madai ya kunywa pombe kupita kiasi.




Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumatano Februari 19,2020 ambapo wananchi wa eneo hilo walivyo amka majira ya saa 12 asubuhi, wakaona mtu akiwa amelala kwenye kibaraza cha moja ya duka kwenye mtaa huo wa Dome akionekana kama amekufa, na walipomsogelea ndipo wakabaini ni kweli amefariki dunia na kutoa taarifa kwa uongozi wa mtaa huo.

Akisimulia tukio hilo, Mwenyekiti wa mtaa wa Dome Solomoni Najulwa, alisema mara baada ya kupewa taarifa na wananchi alifika eneo la tukio na kumkuta kijana huyo amefariki dunia, ndipo akatoa taarifa kwa jeshi la polisi ambapo walifika na daktari wa hospitali ya mkoa kufanya uchunguzi na kubaini pombe ndiyo imemuua.

“Taarifa za awali juu ya kifo cha kijana huyo zilisema ameuawa kwa kupigwa, lakini baada ya daktari kutoka hospitali ya mkoa kufanya uchunguzi imebainika amefariki dunia sababu ya kunywa pombe kupita kiasi,” alisema Najulwa.

Naye daktari kutoka hospitali ya mkoa huo wa Shinyanga  Richard Mwikambe, akiwa eneo la tukio alisema ni kijana huyo hajauawa kwa kupigwa, bali amefariki dunia kwa sababu ya kunywa pombe kupita kiasi, huku akitoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kunywa pombe nyingi jambo ambalo ni hatari kiafya.

Aidha mmoja wa ndugu wa marehemu Machiya Nyambo, alisema ndugu yao huyo alikuwa akifanya kazi za ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali ya Shinyanga mjini, na kubainisha tayari wameshawasiliana na ndugu wengine kutoka Ukenyenge ,ili wafanye taratibu za kuusafirisha mwili na kuuzika.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Deborah Magiligimba alithibitisha kutokea kwa tukio  hilo, na kubainisha hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na jeshi la polisi, ambapo mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa na ndugu zake watakabidhiwa kwa ajili ya mazishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527