MAHAKAMA KUU YA KENYA YATOA AMRI YA KUSITISHWA SAFARI ZOTE ZA NDEGE KUTOKA CHINA KWA HOFU YA CORONA


Mahakama Kuu ya Kenya imetoa amri ya kusitishwa kwa muda ndege zote kutoka China zinazoingia katika nchi hiyo  kufuatia kesi kuhusu virusi vya Corona iliyowasilishwa na chama cha mawakili wa nchi hiyo.

Amri hiyo ya Mahakama Kuu ya Kenya inataka kusitishwa kuingia nchini humo ndege kutoka China kwa kipindi cha siku kumi.

Akitoa hukumu yake leo Jaji James Makau ameziagiza Wizara ya Usalama wa Ndani na ya Afya kuwatafuta abiria wote 239 waliowasili nchini Kenya kutoka China kupitia uwanja wa ndege wa  Kimataifa wa Jomo Kenyata mnamo Februari 26, na kuwatenga katika hospitali ya kijeshi.

Huku hayo yakijiri Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa agizo kuhusu virusi vya Corona kufuatia malalamiko ya umma kutoka kwa Wakenya kuhusiana na jinsi serikali inavyoshughulikia virusi hivyo hatari ambavyo vinaendelea kutikisa mataifa duniani.

Katika agizo lake Rais Uhuru Kenyatta anataka kamati ya kitaifa ya kushughulikia hali ya dharura kushughulikia mlipuko wa virusi vya Corona.

Rais pia ameagiza kukamilishwa kwa kituo cha kitaifa cha kuwatenga na kuwatibu wagonjwa mjini Nairobi katika kipindi cha siku saba.

Magazeti ya Kenya yameendelea kuangazia ghadhabu za Wakenya baada ya serikali kuruhusu ndege kutoka China kutua nchini humo.

Hatua hiyo pia imelalamikiwa sana katika mitandao ya kijamii baada ya ndege ya Shirika la Southern kuwasili nchini Kenya siku ya Jumanne iliyopita na kuruhusiwa kuingia nchini humo abiria 239.

Saa kadhaa kabla ya hatua hiyo, maafisa wa Kenya walikuwa wametangaza kurejeshwa kwa safari za ndege kuelekea China, licha ya hofu ya kusambaa kwa virusi vya Covid-19.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527