HATMA YA KINANA, MAKAMBA NA BERNARD MEMBE BAADA SIKU 7



Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza Kikao cha Usalama na Maadili kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam leo Februari 12, 2020.PICHA NA IKULU

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza Kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CC) kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Chama hicho Lumumba jijini Dar es Salaam leo Februari 12, 2020.

*****

Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimetoa siku saba kwa kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Bernard Membe na kuiwasilisha katika vikao husika.

Kinana na Makamba ambao ni makatibu wakuu wa zamani wa chama hicho na Membe aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania walifika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula kuhojiwa juu ya tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 12, 2020 ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema wanachama hao tayari wamekwisha kuhojiwa na taarifa yao inasubiriwa.

Kinana, Makamba na Membe waliitwa mbele ya kamati ya maadili Desemba 13 mwaka 2019 baada ya sauti zao kuenea katika mitandao ya kijamii wakieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto, uendeshaji nchi na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu huo dhidi ya mtu anayewachafua.

Sauti hizo zilizoanza kusambaa mitandaoni baada ya waraka wa Kinana na Makamba kuutoa Julai 14 mwaka 2019 wakidai uongozi hauwalindi dhidi ya mtu ambaye amekuwa wakiwadhalilisha na ambaye walimwelezea kuwa analindwa na mtu mwenye mamlaka.

Wakati Membe akihojiwa Februari 6, 2020 makao makuu ya CCM, White House jijini Dodoma, Makamba na Kinana wao waihojiwa na kamati hiyo Jumatatu iliyopita ya Februari 10, 2020.

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

TAARIFA KWA UMMA

KIKAO CHA KAMATI KUU MAALUM YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
_______________

Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Lumumba
12 Februari 2020

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kwamba Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imeketi leo Jijini Dar es Salaam chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikao cha Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kimeketi pamoja na mambo mengine kimepokea taarifa zifuatazo; -

Maandalizi ya Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 – 2030 na Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Kamati Kuu imepokea taarifa ya Maendeleo ya Uandishi wa Waraka huu muhimu wa Kisera na kujiridhisha na kazi nzuri ambayo imekwisha kufanyika mpaka ngazi ya Rasimu. Kamati Kuu pia imepitia zoezi la uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na kuagiza maoni ya wadau mbalimbali kujumuishwa na kuzingatia ratiba ya kukamilisha uandishi wake ili vikao vya Chama vifanye uamuzi na kupitisha.

Maombi ya Kujiunga na uanachama wa CCM kutoka kwa Ndg. Fredrick Tluway Sumaye

Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imepokea taarifa ya Maombi ya kujiunga na CCM kutoka kwa Ndg. Fredrick Tluway Sumaye Waziri Mkuu Mstaafu na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Chama na Serikali ambayo imekiletea Chama heshima kubwa na ukubalifu kwa umma wa wananchi, wanachama na viongozi wa vyama vingine vya siasa. Kikao kimempongeza Ndg. Sumaye kwa uamuzi wake, kimeelekeza utaratibu wa kujiunga rasmi katika Chama ufuatwe kwa mujibu wa Katiba ya CCM.

Taarifa ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu

Kamati Kuu imepokea Taarifa ya Awali kutoka kwa Kamati ya Usalama na Maadili juu ya Utekelezaji wa Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) katika Kikao chake cha Mwezi Disemba 2019 Jijini Mwanza kuhusu kuwaita na kuwahoji wanachama watatu, Ndg. Yusuph Makamba, Ndg. Abdulrahman Kinana na Ndg. Benard Membe ambao wote wameshafika mbele ya Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu inayoongozwa na Mzee Philip Mangula, Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara. 

Kamati Kuu imetoa siku saba kwa Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu kukamilisha taarifa inayowahusu wanachama hawa watatu na kuiwasilisha katika Vikao husika.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Imetolewa na,


HUMPHREY POLEPOLE
KATIBU WA NEC – ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527