WAZAZI WA WATOTO WALIOKUWA WAMEPOTEA MBEYA WAKABIDHIWA WATOTO WAO

Na Daud Tiganya

SERIKALI Mkoani Tabora imewakabidhi watoto wawili waliokuwa wamepotea mkoani Mbeya kwa wazazi wao wakiwa na afya njema.


Hatua hiyo inatokana na kupatikana mmoja wao akiwa na mama mmoja Hawa Ally katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega baada ya wasamaria wema kuwa na wasiwasi na mtuhumiwa na kutoa taarifa Polisi.

Akikabidhi watoto hao leo Mkuu wa Mkoa wa Tabora ametoa onyo kwa wale wote wanaohusika na vitendo vya aina hiyo ikiwemo kuiba watoto wachanga na kwamba Serikali itahakikisha inawachulia hatua kali za kisheria.

Aliwataka wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao badala ya kuwategemea wasaidizi wa kazi ndio watumike kuwalea muda mwingi ili kujiepusha na majanga kama haya.

Aidha Mwanri  aliwashukuru wananchi, Jeshi la Polisi kwa ushirikiano wao waliouonyesha na kupelekea kupatikana kwa watoto hao wakiwa na afya njema.

Kwa upande wa baba mzazi wa watoto hao ambaye ni mtumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mashaka Juma baba alisema watoto wake walipotea nmamo Desemba 28 mwaka uliopita.

Alisema mtoto wake mmoja akiwa na miaka mitano na mwingine mwaka mmoja na nusu walipotea wakati yeye na mkewe wakiwa wamekwenda sokoni kununua mahitaji na waliporudi ndipo walipobaini hawapo nyumbani kwao.

Juma alivishukuru vyombo vya habari na viongozo wa mikoa ya Mbeya na Tabora pamoja na wananchi huku akisema bado hajaamini kama kweli watoto wake wamepatikana tena wakiwa hai.

Mama wa watoto hao,Zuhura Kaswa,alisema bado haamini na kwamba alipotaa taarifa za watoto wake kupotea alikuwa akilia na kumuomba Mungu muda wote.

Wakati huo huo mtuhumiwa anayedaiwa kuwatorosha watoto wawili wa mkoani  Mbeya na kumtelekeza mtoto mmoja nyumbani kwa mtu eneo la Chechemi katika Manispaa ya Tabora Hawa Ally anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora Baraka Makona alisema kuwa mtuhumiwa huyo alimuachia mtoto mkubwa mwenye umri wa miaka mitano kwa nyumba ya mkazi wa Chemichemi kwa madai anaenda na mdogo ili kumtafutia matibabu na kuahidi kurudi baadaye.

Alisema mtuhumiwa hakurudi siku hiyo mwishoni mwa mwaka jana,jambo lililomfanya mwananchi aliyetelekezewa mtoto,kutoa taarifa Polisi kesho yake siku ya mwaka mpya.

Baraka aliongeza mtuhumiwa alienda na mdogo hadi Nzega na kumpeleka Hospitali kutokana na kuugua na ndipo ilipogundulika sio mtoto wake na wasamaria wema kutoa taarifa polisi na mtuhumiwa kukamatwa.

Alisema baada ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupata taarifa za kupotea kwa watoto hao,walifuatilia na kugundua mtoto mkubwa katelekezwa Manispaa ya Tabora na mdogo akipatikana Mjini Nzega.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post