WAVUTA BANGI ,WALEVI TISHIO KITANGILI , VIBAKA NGOKOLO.... "TUNAKOMBWA MCHANA", MBUNGE ATAKA VITUO VYA POLISI KILA KATA


Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Julius Masele akizungumza katika kata ya Ngokolo wakati akifanya ziara yake kusikiliza kero za wananchi na kuzungumza na wajumbe wa kamati ya siasa CCM ngazi ya matawi na kata ya Ngokolo leo Januari 5,2020. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkazi wa Ngokolo Rehema Mkono akimweleza Mbunge wake Stephen Masele kero ya vibaka wanaotishia amani katika mitaa ya Ngokolo.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Julius Masele akizungumza katika kata ya Ngokolo na kuahidi kuzungumza na mamlaka mbalimbali ili kuhakikisha changamoto ya vitendo vya uhalifu katika Jimbo lake vinakomeshwa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Songambele katika kata ya Kitangili Madeha Khamis akitoa kero ya wahalifu wanaotishia amani kwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Julius Masele aliyetembelea kata hiyo Januari 4,2019.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Julius Masele akizungumza na wajumbe wa kamati ya siasa CCM ngazi ya matawi na kata ya Kitangiri na kupokea kero mbalimbali za wananchi Januari 4,2020.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Julius Masele akizungumza na wajumbe wa kamati ya siasa CCM ngazi ya matawi na kata ya Kitangili Januari 4,2020.


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Vijana wanaovuta bangi na kunywa pombe aina ya gongo katika kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga wametajwa kuwa tishio na kuchochea vitendo vya ubakaji wa wanawake na watoto,kuvamia watu na kupora mali za wananchi huku vibaka Kata ya Ngokolo wakiwakosesha amani wananchi kwani sasa wanaiba mchana kweupe.

Hayo yamebainika wakati wananchi wakitoa kero zao kwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Masele alipofanya ziara katika kata  17 za Jimbo la Shinyanga kusikiliza kero za wananchi na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kata zilizolalamikiwa kuongoza kwa vitendo vya uhalifu ni Ndala, Ngokolo na Kitangili  katika mitaa ya Songambele,Busulwa na Kitangiri.

Wananchi hao walimweleza Mbunge wao Stephen Masele kuwa katika maeneo hayo wananchi wamekuwa wakiuawa,kuvamiwa na kuibiwa mali zao majumbani huku Jeshi la Polisi likidaiwa kutochukua hatua stahiki kwa wahalifu wanaosumbua mitaani.

 Wakazi wa Kitangili walisema licha ya vijana wanaojihusisha na uvutaji bangi na kunywa pombe aina ya gongo kuwa tishio lakini kila wanapotoa taarifa jeshi la polisi limekuwa likichelewa kufika eneo la tukio na kushindwa kuchukua hatua kwa wahalifu hao.

"Ukubwa wa tatizo la uhalifu Kitangili ni pale tunapowaita polisi pindi panapotokea tukio huwa wanachelewa kufika kwenye matukio. Lakini pia huwezi amini kama kuna polisi wanawajua hao wavuta bangi na wanajua bangi zinakonunuliwa,wakikutana na wavuta bangi mtaani wanaishi vizuri na wavuta bangi ",walisema wananchi hao.

"Mhe. Mbunge hapa Kitangiri kuna tatizo la hawa vijana wanaovuta bangi,vijana hawa wanaovuta bangi hawalimi bangi wapo wanaolima na kuuza bangi na hatujui wanakonunulia bangi. Tunaomba wanaouza bangi wadhibitiwe kwani bangi na gongo ni kichocheo cha masuala ya ubakaji,kuvamia watu na wizi",alieleza Mwenyekiti wa Mtaa wa Songambele Madeha Khamis.

Naye Rehema Mkono mkazi wa kata ya Ngokolo alisema Ngokolo inakabiliwa na changamoto ya vibaka akisema hivi Sasa Ngokolo inazalisha kundi la 'Panya Road' bila kujua ambapo vijana wenye umri chini ya miaka 20 wamekuwa wakifanya vitendo vya uhalifu mchana kweupe kwa kuvizia nyumba za watu na kuiba mali.

 "Ngokolo tunaibiwa mchana na usiku. Mimi mwenyewe nimeibiwa vitu ndani ya nyumba mchana kweupe 'Tunakombewa mchana kweupe' tunaomba tujengewe kituo cha polisi hapa Ngokolo ili kukomesha tatizo hili",alisema Mkono.

Kwa Upande wake,Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Stephen Masele alieleza kusikitishwa na vitendo vya uhalifu vinavyoendelea katika baadhi ya maeneo katika Jimbo la Shinyanga akisema upo umuhimu wa kujenga vituo vya polisi katika kila kata. 

"Katika ziara yangu kutembelea kata 17 za Jimbo la Shinyanga nimepewa taarifa ya vitendo vya uhalifu nitazungumza na mamlaka mbalimbali ili kuhakikisha tunamaliza changamoto hii ili wananchi wetu wawe salama na mali zao",alisema Masele.

Masele  ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika alianza ziara yake kukagua miradi ya maendeleo,kusikiliza kero za wananchi na kuzungumza na wajumbe wa kamati za siasa CCM ngazi ya matawi na kata zote 17 za Jimbo la Shinyanga Mjini kuanzia Desemba 27,2019 na kuhitimisha ziara yake Januari 5,2020.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post