TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE(JKCI) KUJENGA HOSPITALI KUBWA YA MOYO MLOGANZILA

Serikali kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete(JKCI) ikishirikiana na Serikali ya China wanatarajia kujenga hospitali kubwa ya moyo katika eneo la Mloganzila ambapo hatua za awali za mchakato wa ujenzi zimekamilika.


Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof.Mohammed Janabi alieleza kuwa katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano taasisi hiyo imepanua huduma zake na kuboresha huduma za matibabu ya moyo kwa kiwango cha kimataifa.

“Katika kipindi cha miaka minne wagonjwa waliopatiwa huduma ni 300,836 ambao walitibiwa na kurudi nyumbani na wagonjwa 14,960 ambao walilazwa kwa ajili ya kupata matibabu zaidi, na mahitaji yanazidi kuongezeka hata kutoka katika nchi jiraniani”, Alisema Prof.Janabi.

Alisema kuwa mahitaji ya ujenzi wa hospitali kubwa ya Mloganzila yanatokana na kuwepo kwa wagonjwa wengi nje ya nchi ambao wamekuwa wakija kupata matibabu kwa hiyo uwepo wa hospitali hiyo kutaimarisha utoaji huduma za matibabu ya moyo hapa nchini.

Katika kipindi cha Miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano JKCI imeweza kufanya upasuaji mkubwa kwa kusimamisha moyo kwa wagonjwa 1,537 kwa mafanikio makubwa huku vifo vikiwa ni asilimia 6 tu sawa na wagonjwa 92 kitu ambacho kinawashawishi nchi jirani kama Uganda, Rwanda, Malawi, Burundi na Congo DRC kuleta wagonjwa wao kwenye Taasisi hiyo.

Prof.Janabi alisema kuwa uwepo wa vifaa vya kisasa na wataalam waliobobea kumewezesha zoezi la upasuaji kuwa salama,  ambapo upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa kutumia mtambo wa cathlab (catheterization), wagonjwa  4,207 walipata huduma hiyo huku vifo vikiwa ni asilimia 1.3 tu sawa na wagonjwa 42.

“Katika kipindi cha miaka minne huduma za JKCI zimeweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 86 kwa kufanya upasuaji kwa wagonjwa 5,744 ambao wangeenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na uwepo wa vifaa vyenye uwezo mkubwa, hususani kwenye masuala ya upasuaji  wa moyo kwa njia ya tundu dogo” Alisema Prof.Janabi.

Aidha katika kipindi hiki cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, JKCI imeongeza ujuzi wa wataalam ambapo kwa sasa Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kutoa matibabu ya moyo yaliyo salama na kwa wagonjwa wengi ikitanguliwa na Afrika ya Kusini

Aliongeza kuwa JKCI imefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo kwa mtoto mdogo mwenye umri wa siku 7 na mzee mwenye umri wa miaka 101 ambao kwa sasa wagonjwa hao wote wawili wanaendelea vizuri na maisha yao.

“katika kukabiliana na changamoto ya idadi kubwa ya wagonjwa, Rais John Magufuli mwezi Januari 2019 alitoa nafasi kwenye jengo la watoto lililopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kliniki za watoto tu”, Alisema Prof. Janabi.

Prof.Janabi alisema kuwa JKCI imenunua mashine mpya mbalimbali za matibabu ya moyo zikiwemo mashine za kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa umeme wa moyo  unavyofanya kazi, ventilators, cardiac monitors, test gears, mashine ya X-ray pamoja na vifaa vya chumba cha tatu cha upasuaji.

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni hospitali kuu maalum kwa ajili ya matibabu ya moyo inayomilikiwa na Serikali ambayo ilianzishwa Septemba 2015,ambayo imeendelea kuitangaza vyema nchi yetu hata katika nje ya mipaka yetu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527