TCU YAFANYA UHAKIKI NA UTAMBUZI WA VYETI 8328 VYA WAHITIMU WA VYUO VYA NJE

Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) katika kipindi cha mwezi Novemba 2015 hadi Novemba 2019 imefanya uhakiki na utambuzi wa uhalali wa vyeti 8328 vya wahitimu waliotunukiwa tuzo zao na vyuo vikuu vilivyo nje ya Tanzania.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa vyombo vya habari leo Jumanne (Januari 28, 2020) Jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa alisema kutokana na kuimarika kwa  mifumo ya kieletroniki, TCU imefanikiwa kupunguza muda wa  uhakiki na utambuzi wa vyeti hivyo kutoka siku 14 za awali hadi siku tatu.

Prof. Kihampa alisema TCU imeimairisha mifumo yake ya kielektroniki ambayo imeongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa kuboresha huduma inazotoa kwa wateja na wadau wake kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Huduma kwa wateja.

‘’Katika kipindi hiki, zaidi ya maombi 1,077 ya hati ya kutokuwa na pingamizi kwa wanaotaka kwenda kusoma elimu ya juu nje ya nchi, yamewasilishwa TCU na kushughulikiwa na mfumo huu ni muhimu kwani unawapa fursa wananchi kufahamu uhalali wa programu wanazokwenda kusoma, hivyo kuwaepusha kupoteza rasilimali fedha za kusoma katika vyuo visivyotambulika’’ alisema Prof. Kihampa.

Aidha Prof. Kihampa alisema kupitia miongozo yake TCU imeweza kusajili Wakala tatu zinazodahili wanafunzi wanaotaka kusoma elimu ya juu nje ya Tanzania, na kuzitaja wakala hizo ni pamoja na Global Education Link Ltd, DARWIN Education Agency Ltd na Yahoma Educational Ltd, pamoja na kupokea maombi ya wakala nyingine 7 zinazosubiri  taratibu za usajili.

Prof. Kihampa alisema kwa mujibu muongozo huo, wakala wote hutakiwa kuwa na mikataba maalum baina yao na vyuo vilivyopo nje pamoja na Cheti maalum (NOC), na hivyo kuwataka wakala wote waliokidhi vigezo hivyo kutuma maombi yao TCU na kukamilisha usajili kwa wakati.

Katika hatua, nyingine Prof. Kihampa alisema katika kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na vyuo vikuu nchini, kati ya kipindi cha mwezi Oktoba 2016 hadi Januari 2017, TCU  ilifanya ukaguzi maalum wa kitaaluma kwa taasisi 64 za vyuo vikuu, vyuo vikuu vishiriki na vituo vya vyuo vikuu ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa.

‘’Matokeo ya ukaguzi yalibainisha kasoro mbalimbali katika uendeshaji wa vyuo vikuu nchini, vyuo 45 vilikutwa na kasoro ndogondogo, vilipewa ushauri na viliweza kurekebisha katika kipindi kifupi vikaendelea na utoaji wa elimu ya juu na vyuo 19 vilikutwa na kasoro kubwa, vilipewa ushauri na muda wa mrekebisho’’ alisema Prof. Kihampa.

Kwa mujibu wa Prof. Kihampa alisema hadi sasa vyuo vikuu 9 kati ya 19 vilivyositishwa udahili vimefanya marekebisho makubwa na vimeruhusiwa kudahili na kuendelea kutoa mafunzo kwa baadhi ya programu za masomo, na kuvitaja vyuo hivyo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofila Kisanji (TEKU), Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA), Chuo Kikuu Kishirishi cha Marian (MARUCo).

Anavitaja vyuo vingine ni Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala Nchini Tanzania (KIUT), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kikristo cha Tiba Kilimanjaro (KCMUCo), Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stephano- Moshi (SMMUCo) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Mt. Fransisko (SFUCHAS).

Anaongeza kuwa mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara imefanya vyuo kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya kufundisha na kujifunzia ikiwa na pamoja na ujenzi wa maabara za kisasa, mifumo ya mawasiliano ya kielektroniki, madarasa na kuongeza idadi ya viongozi na wahadhiri wenye sifa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post