JAMAA WA MIAKA 50 AUAWA KWA KUPONDWA TOFALI NA MPENZI WAKE WA MIAKA 22 KAHAMA



Na Adela Madyane - Malunde 1 blog Kahama
Mwanaume aitwaye John Maguzu (50) ameuawa kwa kupondwa tofali na mpenzi wake aliyefahamika kwa jina moja la Aneth (22) mkazi wa mtaa wa Majengo kata ya Majengo wilayani Kahama Mkoani Shinyanga  kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.



Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo John Masele amesema kuwa tukio hilo limetokea jana Alhamis Januari 16,2020 majira ya saa mbili usiku wakati Maguzu akiwa katika banda la kitimoto akipata chakula.



"Baada ya Maguzu kumhoji mpenzi wake huyo juu ya mahusiano ya mwanaume mwingine ndipo zilipotokea purukushani na binti kumpiga mpenzi wake na tofali kichwani",aliongeza.



Amesema kutokana na kitendo hicho Mwanaume aliomba msaada kwa marafiki zake ambao walimkimbiza katika Zahanati ya Bakwata ambako alipatiwa huduma ya kwanza lakini kutokana na hali kuwa mbaya rafiki zake walikwenda Polisi na kupewa hati ya matibabu PF3 na kisha kumkimbiza katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama ambako mauti yalimkuta akiwa mapokezi.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, Dkt. George Masasi akithibitisha kupokea mwili huo amesema kuwa majira ya saa 3:30 usiku walipokea mwili wa John Masasi Maguzu (50) mkazi wa mtaa wa Sokola wilayani Kahama.

Dkt. Masasi amesema uchunguzi wa madaktari umebaini kuwa ubongo ulipata hitilafu pamoja na fuvu la kichwa jambo ambalo limepelekea kifo chake na kuongeza kuwa taratibu za mazishi zinaendelea ambapo ndugu wa marehemu walieleza watasafirisha kwenda Badugu mkoani Simiyu kwa ajili ya mazishi.

Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Majengo Vicent Asenga amedhibitisha kutokea kwa tukio hilo katika Kata yake na kusema kuwa alipata taarifa za tukio hilo majira ya saa nane usiku kutoka kwa viongozi wake ngazi ya mtaa huo na lushirikiana nao kumtafuta binti kwaajili ya mahojiano juu ya tukio hilo.

Kwa upande wake Donald Masele ambaye ni balozi katika eneo la makazi ya Maguzu amewataka wananchi kutojihusisha na suala la mapenzi na watu wenye rika kubwa jambo ambalo linaleta madhara makubwa na kutoa ushauri kuwa wanaume wenye umri mkubwa ambao hawana wanawake waoe kuliko kutembea na mabinti wenye umri mdogo.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Joseph Paul amethitisha kutokea kwa tukio hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527