Breaking : MADIWANI WANNE WANAOZUNGUKA MGODI WA MWADUI WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI SHINYANGA...KULALA MAHABUSU LEO



Kushoto ni Diwani wa kata ya Maganzo, Lwinzi Mbalu Kidiga ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madiwani wa kata zinazozunguka mgodi wa Mwadui kulia ni Katibu wa Jumuiya ya Madiwani wanaozunguka mgodi wa Mwadui Abdul Ngolomole ambaye ni Diwani wa Kata ya Songwa (CCM). Picha kutoka Maktaba ya Malunde 1 blog 


Na Waandishi wetu - Malunde 1 blog 
Madiwani wa kata nne za halmashauri ya wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga wanashikiliwa na jeshi la polisi baada ya kutaka kufanya kikao na wenyeviti wa vijiji katika maeneo yao kwa lengo la kujadili manufaa ya Masalia ya mchanga wa madini ya almasi ‘Makinikia’ yaliyotolewa na serikali kwa wananchi kutoka Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond Limited. 

Madiwani wanaoshikiliwa ni Diwani wa kata ya Maganzo Mbalu Kidiga (CCM), kata ya Songwa Abdul Ngoromole (CCM), kata ya Idukilo Sarah Michael (CHADEMA), pamoja na Mwadui Luhumbo Paul Magembe (CHADEMA). 

Imeelezwa kwamba mkutano huo unatokana na kutoridhishwa na maamuzi yaliyotolewa na serikali hivi karibuni kuhusu makinikia hayo ambao ulikuwa ufanyike leo asubuhi Jumamosi Januari 25,2020 uliahirishwa baada askari wa jeshi la polisi kuwazuia madiwani hao na kuwaamuru kuahirisha baada ya agizo kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Kishapu.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamatwa kwa madiwani hao, Wenyeviti wa vijiji kutoka kata hizo wameiomba serikali kuingilia kati kutoa ufafanuzi wa sintofahamu ya mchanga wenye madini ya almasi, unaoibua migogoro kati ya madiwani na Chama Cha Wachimbaji wadogo wa madini mkoa wa Shinyanga (SHIREMA).

Mwenyekiti wa kijiji cha Songwa Damas Francis alisema ameshangazwa na kitendo cha askari wa jeshi la polisi kuingia kwenye kikao na kuwaamuru kuhairisha kikao hicho ambacho ajenda zake zilikuwa kufahamu muafaka wa makinikia utakavyowanufaisha wananchi katika maeneo yao. 

“Nasikitika sana kuvunjiwa mkutano wangu pasipo muafaka wa maana, tulikuja kuzungumzia ni nini nitapata kupitia makinikia katika eneo langu kwa ajili ya kupunguza matukio ya vijana wetu kuvunjwa miguu wakati wanaenda kuiba mchanga wa almasi Mwadui, sasa makinikia hayawalengi wanamzunguko, SHIREMA ni chama cha uchimbaji na makinikia sio uchimbaji kwa hiyo yanawalenga wananchi duni wenye maisha ya chini”, alisema, amesema Damas. 

“Vijiji vya mzunguko takribani vyote havijakamilisha miundombinu ya shule, majengo, madawati hata vyoo hakuna mfano kwenye shule yangu ya sekondari ya songwa haina vyoo, endapo kama gawio la asilimia kutoka mgodini lingekuwepo wala pasingekuwa na tatizo lakini sasa nitapata wapi tena kama hata haya makinikia yenyewe inakuwa ni mvutano namna hii”, ameongeza. 

Mwenyekiti wa kijiji cha Maganzo Charles Manyenye amesema wamekuwa na wasiwasi na hatua zinazochukuliwa na jeshi la polisi na kuhisi uwepo wa maslahi kwa watu wachache wanaotaka kujinufaisha na makinikia hayo. 

“Maaskari wamekuja kwenye eneo la kikao na wakasema kwamba tuahirishe na madiwani wachukuliwe waende Kishapu kuripoti, tukaambiwa kwamba mkuu wa wilaya ndiyo kaagiza hivyo, pengine kuna maslahi ya wakubwa ndiyo labda inapelekea vikao kama hivi vinazuiwa, na sisi hatutakoma tutafikia hatua ya kwenda hadi kwa mheshimiwa wetu rais Magufuli”, amesema Manyenye. 

Aidha mwenyekiti wa kijiji cha Idukilo Patrick Kapela amesema haoni manufaa ya mgodi licha ya kufanyakazi kwa muda wa zaidi ya miaka 50 lakini vijiji vilivyopo jirani na mgodi huo bado havijanufaika na mgao wa asilimia katika uboreshaji wa huduma za kijamii. 

“Huu mgodi una zaidi ya miaka 50 lakini wakazi wa vijiji ya mzunguko hatuoni faida yake, ona sasa na haya makinikia bado wanatukandamiza wakati ilipaswa vijiji vilivyopo kwenye mzunguko kupewa kipaumbele ili angalau vijikwamue na changamoto zilizopo”, amesema Kapela. 

Juhudi za kumtafuta Mkuu wa wilaya ya Kishapu ,Nyabaganga Talaba ili kuzungumzia tukio hilo zinaendelea.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga ACP Joseph Paul amesema wanawashikilia madiwani hao kutokana na kukiuka maagizo ya serikali yaliyotolewa hivi karibuni kuhusu Makinikia. 

"Ni kweli tunawashikilia hawa madiwani,leo waliitisha kikao na wenyeviti wa vijiji na vitongoji tunachunguza kwanza,tukiona wana kosa watapelekwa mahakamani",amesema Kamanda Paul.

Hii ni mara ya pili Madiwani hao kuzuiwa kufanya mkutano ambapo Alhamis Januari 2,2020 katika hali isiyotarajiwa mkutano wa wananchi wanaozunguka Mgodi wa Mwadui ulioandaliwa na Madiwani wanaozunguka mgodi huo kujadili hatima ya Masalia ya mchanga wa madini ya almasi ‘Makinikia’ulipigwa marufuku dakika chache kabla ya mkutano kuanza ambapo ghafla viti viliondolewa huku spika zikizimwa wakati diwani wa Maganzo Lwinzi Mbalu Kidiga akizungumza.

Madiwani hao wa kata zinazozunguka mgodi huo pamoja na wananchi waliokusanyika katika soko la kata ya Maganzo ‘Mji wa Maganzo’ wilayani Kishapu mkoani Shinyanga walitakiwa kutawanyika mara moja kwa madai kuwa ni ‘Order’ Agizo/Amri kutoka juu. 

Hata hivyo, Mvutano wa mgawanyo wa mapato kati ya wachimbaji wadogo wa madini ya Almasi katika kijiji cha Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga na Chama cha wachimbaji wadogo wa madini mkoani Shinyanga (SHIREMA) ulielezwa umemalizika rasmi hivi karibuni katika mkutano wa hadhara uliowashirikisha wachimbaji wadogo, viongozi wa SHIREMA na Rais wa Shirikisho la Vyama vya wachimbaji wadogo wa madini uliofanyika kwenye kijiji cha Masagala kata ya Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Hali ya mgogoro kati ya wachimbaji wadogo na SHIREMA ulijitokeza baada ya serikali kuuagiza mgodi wa Williamson Diamonds Limited wa Mwadui kuwapatia wachimbaji hao masalia ya mchanga wa almasi (makinikia) yaliyomo katika mgodi huo.

Mara baada ya ombi hilo la serikali kukubaliwa,Chama cha wachimbaji wadogo wa madini mkoani Shinyanga kilikabidhiwa jukumu la kuingia mkataba na makampuni yatakayosomba mchanga huo kuutoa nje ya mgodi na kuupeleka katika eneo ambalo wachimbaji watalitumia kuchenjulia almasi.

Hata hivyo mvutano mkubwa uliibuka baada ya wachimbaji wadogo kuelezwa mgao wao katika almasi watakazokuwa wanauza utakuwa ni asilimia 15 huku watoa huduma wakichukua asilimia 80 na SHIREMA asilimia tano.

Kutokana na mvutano huo serikali iliingilia kati mgogoro huo na hatimaye kuupatia ufumbuzi wa kuongezwa kwa kiwango cha asilimia ambazo wachimbaji watapata baada ya kuuza almasi zao ambapo sasa mtoa huduma atapata asilimia 25.

Akitangaza uamuzi huo hivi karibuni, Rais wa Shirikisho la Vyama vya wachimbaji wadogo wa madini nchini, John Bina alisema marekebisho mapya yaliyofanyika yalishirikisha watu wengi ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama na kwamba kwa sasa wachimbaji watapata asilimia 62 badala ya asilimia 15.

“Mabadiliko mapya hivi ni kwamba, kwanza tutatoa asilimia saba ya serikali kama mrabaha, asilimia 0.3 ushuru wa huduma na kinachobaki kitagawanywa kwa mtoa huduma kupata asilimia 25, mwenye shamba, asilimia nane, SHIREMA asilimia tano na mchimbaji sasa atapata asilimia 62,” alieleza Bina.

Rais huyo alisema baada ya marekebisho anaamini mgogoro huo sasa umemalizika na wachimbaji wajipange kwa kuanza kufanya kazi ambapo hata hivyo alionya na kutahadharisha baadhi ya watu wenye tabia ya kuzusha migogoro isiyokuwa na maana kila wakati.

Alisema iwapo wachimbaji hao wataanzisha mgogoro mwingine ni wazi watamvunja nguvu Rais Dkt. John Magufuli ambaye muda wote amekuwa pamoja na watanzania wanyonge na kwamba hata baadhi ya watu watawashangaa kuona kila siku wana migogoro badala ya kuitumia vyema fursa hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post