MAHAKAMA YATUPILIA MBALI KESI YA MBUNGE RWEIKIZA MADAI YA SH BIL. 1 NA MIL 216 KUDHALILISHWA NA KIONGOZI WA CCM


Mdaiwa Mjumbe wa halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Mkoa wa Kagera Novatus Nkwama (mwenye suti katikati) akiwa nje ya jengo la mahakama baada ya hukumu kutolewa

Na Ashura Jumapili - Malunde 1 blog Bukoba
Mahakama  Kuu kanda ya Bukoba Mkoani Kagera imetupilia mbali kesi ya madai namba 12 ya mwaka 2016 ya fidia ya shilingi bilioni 1 na milioni 216 iliyofunguliwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza dhidi ya Mjumbe wa halmashauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Mkoa wa Kagera Novatus Nkwama kuwa alimdhalilisha.

Akisoma hukumu mahakamani hapo jana Jaji wa mahakama hiyo Dk. Ntemi Kilekamajinga ,alidai kuwa baada ya kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili kwanza msingi wa kisheria ni wajibu mdai kuthibitisha madai yake mahakamani.

Jaji Dk. Kilekamajinga alisema katika kesi hiyo aliangalia hoja nne za kesi hiyo ambavyo ni:

1.Je mdaiwa alimdhalilisha mdai?.

2.Maneno yaliyosemwa yalikuwa na udhalilishaji?.

3.Je maneno hayo yalisababisha madhara yoyote ya udhalilishaji/.

4.Maneno ya kushusha hadhi kwa jamii yajulikane na mtu Zaidi ya mmoja.

“Nimechambua ushahidi uliotolewa na mdai yeye hakuwahi kuyasikia maneno ingawa alisikia kupitia kwa watu wakati huo huo anasema alisikia kipindi kikirudiwa katika radio ,anasema kama yeye hakusikia kupitia masikio yake ushahidi wake unaleta ukakasi”,alisema Jaji Dk.Kilekamajinga.

Alisema kifungu cha 62 kifungu kidogo cha (1)cha sheria za ushahidi alitakiwa kuijumuisha Radio Karagwe kwenye ushahidi mahakamani hapo.

Aliieleza mahakama kwamba mdai hakumpeleka mahakamani mtangazaji wa radio hiyo ,wala uthibitisho wowote toka radio Karagwe kwamba ilirusha matangazo yaliyomdhalilisha.

Alisema kuhusu madai kuwa Rweikiza alitukanwa kwenye nyumba ya Nazir Karamagi wakati wa dua mtu anaalikwa kusalimia halafu anaanza kuropoka na kuanza kutukana hilo jambo pia linaleta ukakasi.

Alisema shahidi mwingine wa mdai aliieleza mahakama kuwa akiwa njiani kuelekea bukoba mjini alipita Itawa akasikia mdaiwa anamtukana mdai ,sijui kilichomsimamisha kwa kweli sasa nimejiuliza alitumia usafiri gani kwanza hakuwa pale na ajenda ilikuwa moja ya kujadili wizi katika Kitongoji pia ushahidi wale ni wa ukakasi.

Alisema mashahidi walioileza mahakama kuwa waliacha kazi kwa mdai baada ya kusikia maneno ya udhalilshaji walishindwa kuithibitishia mahakama kama kweli waliacha kazi hawakuleta barua.

Alisema mdai alishindwa kuithibitishia mahakama madai yake ya watoto 50 wa kiislamu waliokuwa wanasoma kwenye shule yake ya ( Rweikiza primary school )walihama baada ya kusikia maneno kuwa anawabagua waislam na kumsababishia hasara kwa sababu hakuleta idadi ya wanafunzi waliokuwepo shuleni kabla ya maneno na waliohama baada ya maneno.

Alisema cha msingi ni uthibitisho wa jambo linalosemwa kwa msingi wa kisheria hivyo kesi hii imejaa msuguano wa kisiasa Zaidi mdai na mdaiwa wanaongalia kugombea mwaka 2020.

Alidai kuwa kwa kutengeneza kesi sababu ya kumuumiza mwingine mahakama haiwezi kuliacha jambo hilo,mahakama imeshindwa kujiridhisha kama kweli maneno hayo yalitolewa na mdaiwa na kama yalitolewa yanaweza kuwa yalikuzwa Zaidi kwa sababu mdai hakusikiliza kwa masikio yake mwenyewe.

Alisema mahakama imeona madai hayana msingi wowote hivyo pande zote mbili ziweze kubeba gharama zake za kesi.

Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo jaji ,huyo alisema kesi hiyo ilishasuluhishwa na chama cha mapinduzi ,viongozi wa serikali na mahakama pia ilisuluhisha ikashindikana ndio ikafunguliwa kesi.

Kesi hiyo ilifunguliwa na mbunge wa jimbo la Bukoba Vijijini Jasson Rweikiza ,akidai fidia ya shilingi bilioni 1 na milioni 216 akidai alidhalilishwa na Novatus Nkwama aliyekuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya Bukoba Vijijini.

Rweikiza ,alisema alitukanwa kuwa yeye ni mwizi alimuibia mdaiwa gari lake,yeye ni mbaguzi anawabagua waislamU na aliiba kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015ndiyo akashinda kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Upande wa mdai ulikuwa na mashahidi 7 na mdaiwa mashahidi 4.

Kwa upande wa mawakili wa upande wa mdaiwa ambao ni Dastan Mujaki na Jovin Rutainulwa walisema wamepokea hukumu kama ilivyotolewa kwa sababu imezingatia haki.

Wakili Mujaki,alisema mahakama hiyo imezingatia misingi ya kisheria kwa kuchambua ushahidi uliotolewa na pande zote mbili na kubaini kuwa kesi hiyo ilitengenezwa.

Alisema liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za kutengeneza kesi na kuwashtaki watu.

Wakili wa upande wa mdai Nyikiza Seth,alitoweka mahakamani hapo bila kuongea chochote hivyo haijajulikana kama wanampango wa kukata rufaa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post