ZITTO KABWE AKANA KUFANYA MAZUNGUMZO YOYOTE NA SUMAYE


Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hawajafanya mazungumzo yoyote na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye leo mchana Jumatano Desemba 4, 2019 ametangaza kuwa si mwanachama wa Chadema.

Zitto ametoa maelezo hayo saa chache baada ya Sumaye kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza sababu za kujiondoa Chadema, moja ikiwa ni hali ya sintofahamu iliyoibuka katika uchaguzi wa uenyekiti Kanda ya Pwani ambao alipigiwa kura 48 za hapana kati ya 76.

Katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Zitto amesema;  "Nipo Mahakamani tangu asubuhi mpaka sasa nikiendelea na kesi ya uchochezi dhidi yangu. Ninasikia tumetajwa tajwa kuhusu Mzee Sumaye. Itoshe kusema kuwa Chama cha @ACTwazalendo  hakina mazungumzo yeyote na Waziri Mkuu huyo Mstaafu. Nashauri apewe nafasi ya kupumzika kama alivyoomba


Sisi kama chama tumehuzunishwa na uamuzi wa Mzee Sumaye kupumzika Siasa. Ilikuwa ni tunu katika upinzani kuwa na Waziri Mkuu Mstaafu katika ngazi zake za Uongozi. Bila shaka tutachota maarifa na uzoefu wake kama mwenyewe alivyoruhusu. Chama chetu kinaheshimu na kuthamini Wastaafu 



 Kwa upande wangu nawatakia kila la kheri wenzetu wa CHADEMA katika Uchaguzi wao unaoendelea. Dhamira yetu ya kuunganisha nguvu ya Vyama vya upinzani ili kukabiliana na CCM haina mashaka. Mara baada ya Uchaguzi wa wenzetu tutaendelea na mazungumzo ya ushirikiano na Uongozi mpya"


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527