BALOZI WA INDONESIA ATUA KAGERA KUSAKA FURSA ZA UWEKEZAJI


Mkuu  wa Mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Marco Gaguti akizungumza na Balozi wa Indonesia nchini  Prof. Ratlan Pardede baada ya kuwasili mkoani Kagera kujionea fursa za uwekezaji.
Na Ashura Jumapili -Malunde 1 blog Bukoba
Wiki ya uwekezaji Kagera imeendelea kuzaa matunda ambapo Balozi wa Indonesia nchini  Prof. Ratlan Pardede amewasili Kagera kujionea fursa za uwekezaji.

Mkuu  wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti, amesema Prof.Ratlan Pardede amefika Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi ili kuangalia fursa mbalimbali za kibiashara ambazo zinaweza kuiunganisha Tanzania na Indonesia.

Alisema kwanza atakutana na Jumuia ya wafanyabiashara mkoani Kagera kwa ajili ya kubadilishana nao mawazo na kuona jinsi watakavyoweza kushirikiana kufanya biashara.

Alisema kwa mkoa ni fursa kubwa kuwa na wawekezaji au mpango wa kuwekeza katika madini ya Tini.

“Tunafahamu siku za nyuma tulipata changamoto kubwa ya watu kujichimbia hovyo hovyo madini ya Tini na tumekuwa tukipambana sana watu wanaotorosha madini haya na kuyapeleka nchi jirani kama tutafanikiwa kupata wawekezaji kutoka nchin Indonesia ambao wapo mbele katika teknolojia watatusaidia sana”,alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Gaguti alisema kwanza watasaidia kuongeza samani ya madini hayo ya Tini hapa nchini pia wanatamani kuuza uzalishaji wa mwisho katika masoko moja kwa moja bila kupitia maeneo mengine.

Alisema itasaidia nchi kupata fedha pia itapunguza adha ya wananchi kutorosha madini hayo kwa njia za panya.

Alisema itatoa fursa kwa nchi jirani kuleta madini yao ili yaweze kuongezewa thamani nchini Tanzania na mapato yataongezeka kwa taifa kupitia madini ya Tini.

Afisa madini mkazi mkoa wa Kagera mhandisi Lukas Mlekwa,alisema Tanzania inahitaji viwanda kwaajili ya kuongeza thamani ya madini ya Tini.

Mhandisi Mlekwa,alisema kwa sasa kuna kiwanda kimoja kilichopo wilayani Kyerwa kunakochimbwa madini hayo na kudai uchimbaji bado uko chini.

Alisema wawekezaji wakifika kuongeza nguvu wakafanya utafiti na kubaini kiwango cha madini ya Tini kilichopo wilayani Kyerwa .
Alisema uchumi wa Kagera utakuwa kwa sababu shughuli zitakuwa ni nyingi,ajira zitaongezeka kwa wakazi wa Kagera hivyo ujio wa balozi wa Indonesia hapa nchin ni muhimu kulingana na changamoto za uchimbaji wa Tini ulipo sasa.

Alisema sheria ya madini inataka madini yote kuongezewa thamani kabla ya kwenda sokoni na kwamba kuna kiwanda kimoja kilichopo Kyerwa cha kuongeza thamani ambacho kimeanza kufanya kazi na pia kinahitajika kiwanda kingine.

Alisema viwanda vikiwa karibu changamoto za utoroshaji wa madini hayo kwenda nchi jirani itaisha.

Alisema itasaidia madini yanayochimbwa na wacimbaji wadogo yataelekezwa kwenye kiwanda kwaajili ya mchakato wa kuongeza thamani na changamoto zitapungua.

"Mkoa wa Kagera una madini mengi ambayo hayajafanyiwa utafiti yanahitaji wawekezaji wengi. Mkoa una jumla ya leseni 655 za wachimbaji wadogo wa madini yote yanayopatikana mkoani Kagera. Leseni za tini 257 za wachimbaji wadogo na leseni 26 za utafiti ",alisema.

Kwa upande wake balozi wa Indonesia nchini Tanzania Prof. Ratlan Pardede ,baada ya kuelezwa fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Kagera ,alijikita kwenye eneo la madini ya Tini yanayopatikana katika wilaya ya Kyerwa pekee nchi nzima.

Prof.Pardede,alisema India kuna uzoefu wa kutosha upande wa madini ya Tini.

Hata hivyo balozi huyo amekwenda Wilayani Kyerwa kujionea hali halisi ya uchimbaji wa madini ya Tini wilayani humo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527