LIUNDI : WAANDISHI WA HABARI ANDIKENI SIMULIZI ZA WANAWAKE WALIOSHIKA NAFASI ZA UONGOZI



Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Lilian Liundi
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Waandishi wa habari wametakiwa kutumia kalamu zao kuwapa nafasi kwenye vyombo vya habari wanawake waliothubutu kupata nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo siasa ili waweze kutoa simulizi za mafanikio yao na changamoto walizopitia wakitekeleza majukumu yao.


Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Desemba 18,2019 na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) Lilian Liundi wakati wa warsha ya kuvuna matokeo kutoka kwa waandishi wa habari wa mikoa mbalimbali nchini waliopewa mafunzo juu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi ikiwemo siasa. 

Liundi alisema ili kufikia usawa wa kijinsia moja ya jukumu kubwa la waandishi wa habari ni kuandika habari za simulizi za wanawake mashujaa walioshika nafasi za uongozi ili wanawake wengine wahamasike, wawe na ujasiri wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii.

“Hawa viongozi wanawake waliopo wapeni nafasi, sikilizeni simulizi zao dunia ijue ili wale waliokata tamaa wapate ujasiri wa kugombea nafasi za uongozi. Wapo waliopitia changamoto nyingi ikiwemo mila na desturi kandamizi hadi kufikia hapo walipo hivyo simulizi zao zitasaidia kujenga wengine”,alisema Liundi.


“Wasikilizeni wanawake mashujaa,ongeeni na wanawake walioshinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,madiwani,wabunge na viongozi wengine,wapeni moyo na kuwatia moyo wasikatishwe tamaa”,aliongeza Liundi.


Katika hatua nyingine Liundi alisema masuala ya jinsia ni mambo ya maendeleo hivyo yanapaswa kupewa kipaumbele ili kuleta maendelo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Liundi alitumia fursa hiyo kutambulisha Ilani ya uchaguzi ya wanawake iliyoandaliwa na TGNP Mtandao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali huku akibainisha kuwa taifa linahitaji watu wote bila kujali kuwa ni mwanamke,mlemavu ama mwanaume wafaidi nafasi za uongozi.

Kwa upande wake,Afisa Programu Mwandamizi wa TGNP Mtandao, Deogratius Temba alisema lengo la TGNP kutengeneza Ilani ya Uchaguzi ya wanawake (Uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020) ni kubeba ajenda ya mwanamke ili kuhakikisha wanawake wanapata nafasi za uongozi katika nyanja zote na kushiriki katika ngazi za maamuzi.

“Ilani ya uchaguzi ya wanawake ya mwaka 2019/2020 imeweka masuala muhimu ya jinsia katika uchaguzi. Ilani hii inazitaka mamlaka zote kuzingatia masuala ya jinsia katika uchaguzi”,alisema Temba. 

"Ilani hii pia inataka wadau wote wa uchaguzi wanazingatia misingi ya ushindani wa haki na huru na usawa wa jinsia kama ilivyoainishwa kwenye katiba,sheria,sera,mipango ya nchi na kubainishwa kwenye mikataba ya kimataifa na kikanda ambayo serikali yetu imeridhia",aliongeza Temba. 

Aidha aliwataka waandishi wa habari waandike habari nzuri zisizodhalilisha wanawake, kutoa fursa kwa wagombea wanawake ili waweze kujinadi kwa wapiga kura kwa bei nafuu na kuepuka tabia ya kuwadhalilisha wanawake kwenye vyombo vya habari.

Nao Washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru TGNP Mtandao kwa kuwajengea uelewa na uwezo kuhusu masuala ya jinsia na kwamba watatumia kalamu zao kuielimisha jamii kuhusu haki za wanawake na kutoa fursa kwa wagombea wanawake pamoja na kutoa kipaumbele kuhabarisha jamii kuhusu matukio yenye jumbe za utetezi wa wanawake.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyolenga kuwajengea na kuongezea uelewa na uwezo wa kuripoti masuala ya kijinsia hasa katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana kwenye uongozi yamefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Silver Paradise Hotel jijini Dar es salaam na kukutanisha waandishi wa habari kutoka mikoa ya Shinyanga,Rukwa,Kilimanjaro, Ruvuma,Pwani,Morogoro na Dar es salaam.


ANGALIA PICHA HAPA CHINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP Mtandao) Lilian Liundi akizungumza wakati wa warsha ya kuvuna matokeo kutoka kwa waandishi wa habari wa mikoa mbalimbali nchini waliopewa mafunzo juu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi ikiwemo siasa leo Jumatano Desemba 18,2019 katika ukumbi wa Silver Paradise Hotel jijini Dar es salaam.Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog. 
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Lilian Liundi akiwahamasisha waandishi wa habari kuandika habari zenye mrengo wa kijinsia.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao Lilian Liundi akiwahamasisha waandishi wa habari kufanya mahojiano na wanawake mashujaa waliothubutu kugombea nafasi za uongozi ili watoe simulizi na wasifu wao kwa ajili ya kuhamasisha waliokata tamaa wagombee nafasi za uongozi.

Afisa Programu Mwandamizi wa TGNP Mtandao, Deogratius Temba akitoa mada kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya wanawake (Uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020).
Afisa Programu Mwandamizi wa TGNP Mtandao, Deogratius Temba akiendelea kuwasilisha mada ambapo alisema ushindi wa wanawake kwenye uchaguzi utategemea sana uamuzi wa wapiga kura,wake kwa waume hivyo ni vyema kuwapa moyo wanawake wanaojitokeza kuwania viti vya uchaguzi na kushawishi vyama vya siasa kuteua wanawake wenye uwezo kuwania nafasi za uongozi.

Afisa Habari wa TGNP Mtandao,Monica John akizungumza wakati wa warsha ya kuvuna matokeo kutoka kwa waandishi wa habari wa mikoa mbalimbali nchini waliopewa mafunzo juu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi ikiwemo siasa.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.

Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Shinyanga,Rukwa,Kilimanjaro, Ruvuma,Pwani,Morogoro na Dar es salaam wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufungwa kwa warsha ya siku mbili ya kuvuna matokeo kutoka kwa waandishi wa habari waliopewa mafunzo juu ya ushiriki wa wanawake katika uongozi katika ukumbi wa Silver Paradise Hotel Jijini Dar es salaam kuanzia Desemba 17,2019 hadi Desemba 18,2019.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527