TRA YAWAONYA VISHOKA WANAORUBUNI WALIPA KODI
Na Shushu Joel

MAMLAKA ya mapato Tanzania (TRA) imetoa tahadhari kwa baadhi ya watu maarufu kama Vishoka wanaojifanya kuwa ni Watumishi wa mamlaka hiyo  kwa tabia za kuwarubuni Walipakodi.


Tahadhari hiyo imetolewa jana na Afisa wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Bw. Christian Kyomushula Jijini Dar es Salam.

Akizungumza na baadhi ya Wafanyabiashara wa maeneo hayo alisema kuwa, kumekuwepo na watu katika maeneo hayo wenye kuwarubuni wafanyabiashara kwa kuwaambia kuwa wao ni Maafisa wa TRA hivyo wanauwezo wakuwasaidia ili mambo yao yaende safi.

"Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ipo makini katika kuwatumikia wanyonge hivyo niwaonye wale wote wenye tabia za kujifanya ni watumishi wa TRA wakati sio kweli kuacha mara moja kwani wakikamatwa tutawafikisha katika Vyombo vya Sheria", alisema Kyomushula.

Aliongeza kuwa, wengi wao wamekuwa  wakidanganywa juu ya upatikanaji wa Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) kuwa inatolewa kwa malipo fulani wakati sio kweli, sisi hatuuzi TIN bali tunazitoa bure kwa watu waliokidhi vigezo vya kupatiwa.

Aidha, amewataka wafanyabiasha hao kuendelea kujitokeza kwa wingi katika kushiriki kampeni ya elimu kwa Mlipakodi ili waweze kupata elimu zaidi kuhusu masuala ya kodi na waweze pia kusajiliwa na kupewa TIN.

Kwa upande wake Bw. Karim Kalembo ambaye ni Mfanyabiashara wa samani za ndani alisema kuwa, hapo awali walikua na wakati mgumu kutokana na kuwaona Maafisa wa TRA kama Polisi lakini kipindi hiki TRA wamekuja na kampeni kabambe ya wa uelimishkwa walipakodi.

Aliongeza kuwa wafanyabiashara tumekuwa marafiki na TRA kutokana kwamba wao TRA  wamekuwa karibu sana nasi kwa kutuelimisha .

Naye Bw. Billian  Enok mfanyakazi wa Kituo cha kuuza Mafuta ameipongeza TRA kwa ufanisi wake wa utoaji wa elimu kwa walipakodi .

Alieleza kuwa katika shughuli zao za uuzaji wa mafuta changamoto kubwa ni ya vijana wa bodoboda kutokuchukua risiti pindi wakimaliza kuwekewa mafuta.

Aidha ameiomba TRA kuendelea kutoa elimu kwa vijana hao ili waweze kutambua thamani ya kudai risiti pindi wanaponunua mafuta.


TRA imejikita kutoa elimu ya kodi na kuwahudumia Walipakodi ikiwemo kuwasajili ambapo imekuja na Kampeni kabambe ya wiki mbili kwa mkoa wa Dar es Salaam na zoezi hilo ni endelevu kwa mikoa mingine Tanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post