ALIYEACHIWA KWA MSAMAHA WA RAIS MAGUFULI AUAWA BAADA KUUA MFUNGWA NA KUCHOMA WATU VISU STENDI

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera ACP Revocatus Malimi

Na Ashura Jumapili - Malunde 1 blog

Mfungwa aliyeachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Pombe Magufuli kutoka gereza la Bukoba mkoani Kagera amevamia stendi kuu ya mabasi na kuwachoma watu visu na kusababisha kifo mfungwa mwenzake aliyeachiwa kwa msamaha na kujeruhi wananchi wengine watano kisha wananchi wenye hasira kali kujichukulia sheria mkononi kumuua pia.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera Revocatus Malimi amesema tukio hilo limetokea Desemba 13 ,2019 majira ya saa tatu usiku eneo la stendi kuu ya mabasi katika Manispaa ya Bukoba.

Amesema kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa ghafla mtu mmoja asiyefahamika majina yake mwenye umri kati ya miaka (30-35 ) alivamia maeneo ya stendi hiyo na kumchoma kisu tumboni na usoni Godfrey Gobadi ( 35 ) dereva wa bajaji na kumsababishia kifo papo hapo ambaye pia aliachiwa kwa msamaha wa Rais.

Amesema mtu huyo alizidi kusababisha hofu na taharuki kubwa kwa watu katika eneo hilo alipoendelea kuvamia na kuwachoma kisu watu wengine na kujeruhi wananchi  watano.

Kamanda Malimi amewataja waliojeruhiwa kuwa ni Michael Bukerebe (26 ) kutoka Mwanza ambaye ni fundi magari amejeruhiwa maeneo ya shingoni na mgongoni,Salum Athuman (35 ),mkazi wa Omukigusha Bukoba ,amejeruhiwa mbavuni na mkononi,Jalia Abdi (40 )na mkazi wa Migera Bukoba wakala wa magari amejeruhiwa mgongoni,Jimmy Mashaeli (45 ),amejeruhiwa mikono yote miwili na Nasri Abdalah (19 )Mdigo fundi Magari mkazi wa Dar essalaam .

Amesema baada ya mtuhumiwa kufanya vitendo hivyo ,wananchi wenye hasira kali walimvamia na kuanza kumshambulia na kumuumiza vibaya.

"Askari polisi waliokuwa doria na waliokuwa kituoni waliwahi katika tukio hilo na kufanikiwa kumuokoa mtuhumiwa asiendelee kushambuliwa lakini alifariki wakati akipelekwa hospitali",amesema Kamanda Malimi.

"Uchunguzi wa Awali umebaini kwa mujibu wa karatasi “Discharge form”iliyokuwa mfukoni yenye majina ya ( EX –CONV 655/2019 Godfrey Gobadi ,iliyokuwa katika mfuko wa nguo zake ni ya marehemu huyo iliyomtoa gerezani kwa msamaha wa Rais John Pombe Magufuli".

Amesema mtuhumiwa aliyeuawa na wananchi hakuwa na kitambulisho chochote na ametambuliwa kwa asilimia 60 kuwa naye alitoka gereza la Bukoba kwa msamaha wa Rais na kwamba chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Bukoba mkoani Kagera Dk.Mussa Sweya amesema Desemba 13 mwaka huu majira ya saa 3:30 usiku alipokea marehemu wawili wa kiume na majeruhi watano.

Dk .Sweya,amesema kati ya marehemu wawili aliowapokea mmoja alitambuliwa kwa jina la Gerofrey Kobadi na mwingine hajatambuliwa.

Amesema majeruhi wawili walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka kutokana na kuwa na majeraha madogo na watatu walilazwa kwa ajili ya uangalizi wa karibu.

Amewataja waliolazwa kuwa ni Michael Bukerebe (26 ),Salum Athuman (35 ) na Nasri Abdalah (19 ) na kusema kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

Amesema Sulum Athuman alifanyiwa upasuaji mkubwa uliochukua muda wa masaa matano na kudai kuwa hali yake inaendelea kuimarika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527