KAULI YA MBOWE LIVE MBELE YA RAIS MAGUFULI KWENYE MAADHIMISHO YA MIAKA 58 YA UHURU 'KILIO CHA DEMOKRASIA'



Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowea,amehudhuria maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru katika Uwanja wa CCM Kirumba,jijini Mwanza.



Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hakuvaa sare maalum za chama wala kombati ambazo zinatumiwa kama vazi maalum chama chao lakini amepigilia suti nyeusi, shati jeupe na tai. Viongozi wengine wa CHADEMA,CUF na vyama vingine vya siasa wamehudhuria maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru na miaka 57 ya Jamhuri.


Akizungumza baada ya Rais Magufuli kuwakaribisha viongozi wa vyama vya siasa waliokuwa wamekaa jukwaa kuu kusalimia wananchi,Mhe. Mbowe ametoa kauli zifuatazo:


"Nimekuja kuhudhuria maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru kama Uthibitisho wa Ulazima wa uwepo wa maridhiano,uwepo upendo,uwepo mshikamano katika taifa letu.

Nawapongeza sana Watanzania kwa siku ya leo na namuomba Mwenyezi Mungu siku ya leo ikafungue milango tuweze kuishi kama taifa la watu wanaopendana,tuvumiliane,tukosoane turuhusu demokrasia tujenge taifa lenye upendo na mshikamano 

Na Mhe. Rais kwa nafasi ya pekee tuna nafasi ya kuweka historia ya maridhiano katika taifa kwani kuna wengine wanalalamika,wengine wanaumia,Mhe. Rais tumia nafasi ukaliweke taifa katika hali ya utengamano" - Mbowe



Akitumia salaam ya chama chake cha “Haki” Mwenyekiti wa CUF ,Profesa Lipumba amesema pamoja na hatua kubwa ya maendeleo inayopigwa, ni jukumu na wajibu wa Rais Magufuli na Serikali kuendeleza misingi ya demokrasia nchini.


Viongozi wengine waliotoa salaam na kusisitiza mshikamano, umoja na ulinzi wa amani ya Taifa ni mwenyekiti wa UDP, John Cheyo na mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya siasa, John Shibuda.

Taarifa ya kushiriki kwenye maadhimisho kwa Mwenyekiti wa CHADEMA ilitolewa juzi na Kamati Kuu ya chama hicho kwa kumuagiza Mwenyekiti wake kwenda kukiwakilisha chama hicho kwenye Sherehe hizo za Uhuru.

 Hii ni mara ya kwanza kwa CHADEMA kushiriki kwenye maadhimisho ya Uhuru tangu mwaka 2015.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527