TANZANIA IMEPOTEZA MAJENERALI WA SEKTA BINAFSI


Pichani juu kushoto ni Elvis Tables Musiba, Ali Mufuruki na pichani chini kulia ni Sir. Andy Chande, Ruge Mutahaba pamoja na Dkt. Reginald Mengi enzi za uhai wao.

Na Paul R.K Mashauri
Miaka michache iliyopita tulimpoteza Elvis Tables Musiba aliyekuwa Mwenyekiti wa TPSF (Tanzania Private Sector Foundation). Mwaka jana tukampoteza Sir. Andy Chande aliyekuwa kiongozi wa sekta binafsi toka enzi za ukoloni. Mwaka huu tumewapoteza wafanyabiashara 3 wakubwa ambao walikuwa viongozi na watu muhimu sana kwa sekta binafsi Tanzania. Dr. Reginald Abraham Mengi aliyekuwa Mwenyekiti wa CTI (Confederation of Tanzania Industries) na TPSF, Ruge Mutahaba aliyekuwa mjumbe wa MOAT (Media Owners Association of Tanzania) na mjumbe wa TRA Stakeholders Forum na jana tumempoteza Mr. Ali Mfuruki aliyekuwa Mwenyekiti wa CEO Round Table.

Vijana wengi wamewaona na kuwasikia hawa watu "the generals" lakini wengi hawajui historia ya sekta binafsi Tanzania na mchango wao katika kuifikisha sekta binafsi hapo ilipo. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipoeleza japo kwa kifupi mchango wao kwa sababu kwa namna moja au nyingine wote hawa kuanzia Sir. Andy Chande, Elvis Tables Musiba, Dr. Reginald Abraham Mengi, Mr. Ali Mfuruki na Ruge Mutahaba nimefanya nao kazi za sekta binafsi kwa karibu sana.

Sir. Andy Chande nilifanya naye kazi akiwa ni Mwenyekiti wa "boards" mbalimbali za taasisi kama MOI, IMTU, TRL nk. Na pia alikuwa mshauri katika "board" ya kampuni yangu mwenyewe. Ni bahati mbaya sana kwamba mwezi moja kabla ya kifo chake, mimi na Sir. Andy Chande tulipanga kukutana ili mimi Paul Mashauri nimfanyie "interview" ya namna sekta binafsi ya nchi hii ilivyokuwa kabla na baada ya uhuru. "Interview" ile ilikuwa itumike kama kipindi cha TV ili wengi zaidi wanufaike na uzoefu aliokuwa nao. Bahati mbaya Sir. Andy Chande alifariki kabla hatujakamilisha jambo hilo jema.

Elvis Tables Musiba nilifanya naye kazi akiwa Mwenyekiti wa TPSF na mimi nikiwa mjumbe wa kamati mbalimbali za sekta binafsi Tanzania. Tulisaidiana kuchangisha fedha"fundraising" kwa shughuli mbalimbali za kitaifa, na alitumia wakati huo kunisimulia mambo mengi sana.

Mr. Ali Mfuruki nilifanya naye kazi akiwa ni Mwenyekiti wa CEO Round Table na mlezi wa TRBN (Tanzania Responsible Business Network) chini ya UN Business Compact na mimi nikiwa ni mjumbe wa "secretariat" ya TRBN.

Dr. Reginald Abraham Mengi nilifanya naye kazi yeye akiwa ni Mwenyekiti wa CTI na mimi nikiwa ni mjumbe wa kamati ya SME ya CTI. Na Ruge Mutahaba nilifanya naye kazi wote tukiwa wajumbe wa TRA Stakeholders Forum.

Mara nyingi wote hawa walitumia muda wao mwingi kunisimulia vitu vingi sana wao wakiwa wakubwa kwangu kiumri na mimi nikiwa mdogo sana kwao. Wakati huo nilikuwa sijui kwanini wananiambia mambo yote hayo ya sekta binafsi kwa sababu kwanza nilikuwa mdogo sana na pili sikuwa na nafasi wala heshima kubwa kama walizokuwa nazo wao lakini jana baada ya kupata taarifa za kifo cha Mr. Ali Mfuruki nikagundua pengine walitaka siku moja niyasimulie hayo ili kizazi cha leo kipate kuelewa.

Wafanyabishara vijana, viongozi vijana katika serikali na wajasiriamali vijana wanaochipukia, lazima waelezwe kwamba historia ya sekta binafsi Tanzania haiwezi kuelezwa pasipo majina ya hawa wote niliowataja hapo juu. Lakini pia wapo wengine ambao wameshatutoka na wengine ambao bado wapo hai. Pia sitatenda haki nisipowataja japo baadhi yao. Hao ni pamoja na marehemu Mzee Mwakitwange, Dr. Reginald Abraham Mengi, Mzee Anorld Kileo, Dr. Juma Mwapachu, Elvis Tables Musiba, Mzee Iddi Simba na wengine ambao sikupata kuwafahamu. Hawa walikuwa waanzilishi wa TCCIA mwishoni mwa miaka ya 80 kabla ya baadhi yao kuondoka TCCIA na kuanzisha CTI. Kwanini waliondoka na TCCIA kuanzisha CTI? Hiyo ni mada nyingine ambayo inahitaji makala tofauti na hii.

Ukiondoa Mzee Mwakitwange ambaye alitangulia mbele za haki zamani kidogo, wengine wote akiwemo Mzee Anorld Kileo, Dr. Juma Mapachu na Mzee Iddi Simba nimepata kufanya nao kazi na kupata simulizi zao. Mzee Anorld Kileo ambaye alikuwa ni CEO wa TBL kwa muda mrefu sana na kiongozi wa TPSF yeye aliniita ofisini kwake na kunikalisha chini kwa masaa zaidi ya 3 akinieleza sekta binafsi ilipotoka na namna walivyopambana kuifikisha hapo ilipo. Ukurasa huu hautoshi kuandika historia yote ya ujasiriamali Tanzania ambayo vijana wengi wangependa kuijua lakini Dr. Juma Mwapachu aliandika kitabu chenye historia hii vizuri sana. Mimi nitagusia yale niliyoelezwa na hawa "generals" wa sekta binafsi Tanzania kwa kifupi sana.

1.     Sir. Andy Chande, Mwanzilishi, Chande Mills

Sir Andy Chande alinieleza kwamba baada ya Uhuru wa nchi hii, Rais wa kwanza wa Tanzania Mwl. Julius K. Nyerere alitaka kumteua kwenye baraza la mawaziri. Lakini akamwambia Mwalimu Nyerere, naomba uniache kwenye sekta binafsi. Mwalimu Nyerere aliheshimu mawazo ya Sir. Andy Chande. Lakini Mwalimu Nyerere akaamua kumteua Sir. Andy Chande kuwa mjumbe wa kamati ya uchumi na maendeleo mara tu baada ya Tanzania kupata uhuru. Kwa vijana wasiomfahamu Sir. Andy Chande huyu ndiye aliyekuwa mfanyabiashara wa kitanzania mwenye nguvu kubwa za kiuchumi wakati wa ukoloni na hata baada ya kupata uhuru. Aliendesha biashara ya kifamilia iliyoitwa Chande Mills ambayo baadaye ilitaifishwa na serikali mwaka 1967 wakati wa "Nationalization" na kuwa NMC (National Milling Corporation) kiwanda ambacho baadaye kilikuja kununuliwa na Bakhresa.

Sir. Andy Chande ndiye aliyekuwa mtanzania mwenye asili ya kiasia kuanza kutoa misaada kwa watu (philanthropism) kuanzia wakati wa uhuru mpaka alipofariki dunia miaka michache iliyopita. Kilichonishangaza kuhusu Sir. Andy Chande ni kwamba hata baada ya serikali kutaifisha biashara yake, bado aliendelea kutumia mtandao wake wa watu "network" akili na maarifa yake kuitumikia nchi. Sir. Andy Chande ananisimulia anasema, baada ya serikali kutaifisha biashara yake, Mwalimu Nyerere alimuita Ikulu, akamuuliza; Rafiki yangu Chande; unataka kwenda wapi baada ya serikali kuchukua biashara yako kwa manufaa ya umma?

Sir. Andy Chande akamuambia Mwalimu Nyerere; "sina pa kwenda". Mwalimu akamuambia "sasa kuanzia leo, wewe ndio utakuwa Mwenyekiti wa bodi ya kampuni hii mpya inayomilikiwa na wananchi wote wa Tanzania. Sir. Andy Chande akajibu " sawa Mh. Rais". Na ikawa hivyo. Ingekuwa sisi vijana wa leo, rafiki yako ndiyo kiongozi wa nchi au DC au Mkuu wa mkoa au Waziri, anakufahamisha maamuzi ya serikali, tungeleta urafiki na mambo binafsi kwenye mambo ya nchi. Lakini Sir. Andy Chande alikuwa anajua kutofautisha ni wakati gani Nyerere, "rafiki" yake anaongea na ni wakati gani Nyerere, "Rais wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu" anaongea. Alikuwa anajua mipaka yake.

Kutokana na uwezo wa Sir. Andy Chande, Mwalimu Nyerere alimpa uenyekiti wa "boards" nyingi sana ikiwa ni pamoja na TRL, ATC nk. Pia alikuwa Mwenyekiti wa "board" ya Kioo Ltd, Shaaban Robert Secondary School, IST, Barclays bank, Taasisi ya walemavu buguruni nk. Siwezi kuzimaliza zote ni nyingi mno.

Nilikuwa nyumbani kwake Upanga alipokuwa akisimulia haya. Nikamuuliza sasa uliwezaje kukubali kuwa Mwenyekiti wa "board" ya kampuni ambayo umeihangaikia miaka mingi na sasa si yako tena. Akasema mke wangu alinitia sana moyo. Lakini pili kwenye biashara usiweke mambo moyoni. Ukiweka mambo moyoni utakufa. Moyoni nikajisemea; Huyu kampuni yake aliyoisotea miaka mingi imechukuliwa. Tena siyo kampuni yenye mapato ya shilingi milioni 10 au bilioni moja. Unazungumzia mabilioni ya shilingi. Lakini bado maisha yakaendelea. Wewe umepoteza mteja mmoja unataka kufunga biashara. Kwanini? Hayo ni masomo ambayo nataka vijana wengi wayashike, kwamba;

      I.          Mke au mume wako ana mchango mkubwa sana katika maisha yako ya uongozi, biashara au ujasiriamali. Unapooa au kuolewa lazima uangalie mtu ambaye atakutia moyo wakati ukipitia changamoto za maisha kama ilivyokuwa kwa Sir. Andy Chande. Sio mke au mume ambaye atakukimbia ukifilisika au ukifilisiwa au ukishushwa cheo au ukifukuzwa kazi.

Wakati Sir. Andy Chande akiniambia haya, mke wake alikuwa ni mgonjwa na alikuwa anapata matibabu nchini Uingereza. Pamoja na umri wao mkubwa walipendana sana na kutiana moyo. Na mara nyingi nilipowatembelea niliona Sir. Andy Chande akimhudumia mke wake kwa hali na mali. Kipindi hicho pia Sir. Andy Chande naye hali yake ya kiafya haikuwa nzuri lakini hakuacha kufanya kazi. Alikuwa akiandika makala katika magazeti mbalimbali ya Uingereza na Canada. Sir. Andy Chande alikuwa rafiki mkubwa wa familia ya Malkia wa Uingereza-Qeen Elizabeth, Waziri mkuu wa Canada, na Marais wastaafu akiwemo Mh. Rais Ali Hassan Mwinyi, Mh. Rais Benjamin Mkapa na Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

    II.          Somo la pili ni kwamba ukiwa mfanyabiashara au mjasiriamali, usiweke mambo moyoni, utakufa. Sir Andy Chande na Mwalimu Nyerere walikuwa ni marafiki wakubwa. Lakini maamuzi ya kutaifisha biashara ya Sir. Andy Chande hayakufanywa na mwalimu kama "mtu binafsi" ingawa yeye alikuwa ni mkuu wa nchi. Yalifanywa na serikali. Iwe yalikuwa ni maamuzi mazuri au mabaya, Sir. Andy Chande aliyapokea na kuyaunga mkono. Urafiki wao uliendelea na yeye aliendelea na maisha kama vile hakuna lililotokea.

Leo ukimkopa rafiki yako hela akakuambia hana hela za kukusaidia au hawezi kukupa ana mipango na hela alizonazo, una "mdelete" mpaka kwenye simu yako, "unamblock" facebook, "unamunfollow twitter, instagram na youtube". Ukimpigia simu rafiki yako asipopokea mara 2 au mara 3, unatuma ujumbe mfupi; "acha ujinga pokea simu" hata hujui kama yuko hospitali-ICU kalazwa au bafuni anaoga.
Uko wapi ujasiri wa akina Sir. Andy Chande katika kizazi cha leo? Iko wapi nidhamu ya akina Sir. Andy Chande katika kizazi cha wakati huu? Sir. Andy Chande ananiambia wakati akiwa na Chande Mills, mama Maria Nyerere alikuwa akienda kiwandani kuchukua mabaki ya mahindi kwa sababu alikuwa anafuga. Akasema mama Maria alikuwa hataki akifika kiwandani apewe "priority" wengine wasubiri. Alikuwa anapanga foleni kama wanawake wengine. Hata yeye alipojaribu kumshawishi ahudumiwe kwanza alikataa. Vijana wa leo ambao ni viongozi jifunzeni kitu hapa kutoka kwa mama Maria Nyerere. Wake au waume zenu wajishushe. Wasitake kupewa "priority" kwa sababu tu ni wake au waume wa viongozi. Akienda benki au saloon, mwambie na yeye apange foleni kama wengine. Ndio watu wakubwa "great people" wanavyoishi. Hawana makuu ingawa ni wakuu.

2.     Elvis Tables Musiba, Mwenyekiti wa zamani, TPSF

Nikiwa mtoto mdogo nilikuwa nasoma vitabu vya Elvis Tables Musiba. Moja kati ya vitabu ambavyo sitopata kuvisahau ni kitabu kinachoitwa NJAMA. Kitabu kile cha kipelelezi kilikuwa kina "character" anaitwa Willy Gamba. Ulikuwa ukisoma vitabu vya Elvis Tables Musiba ni kama unaangalia sinema ya Rambo. Nakumbuka nilipokinunua kitabu kile sikulala usingizi mpaka nilipokimaliza. Willy Gamba alikuwa mtu hatari sana ndani ya ile simulizi. Na Elvis Tables Musiba alikwa ni gwiji na mwandishi mkubwa na mzuri sana. Kila ninapokutana na rafiki yangu Eric James Shigongo ambaye pia ni mwandishi wa vitabu namkumbuka Elvis Tables Musiba. Siku moja nitamuuliza Eric James Shigongo alipata wapi hamasa ya kuandika vitabu. Inawezekana alisoma pia vitabu vya Elvis Tables Musiba.

Nilipokutana na Elvis Tables Musiba nilishangaa kugundua kuwa alikuwa ana kipaji kingine cha biashara na uongozi. Wakati tunachangisha fedha kwa ajili ya kongamano moja katika sekta ya utalii, aliniita ofisini kwake Mirambo House karibu na ofisi za benki ya dunia. Tulikuwa tunahitaji kuchangisha kama shilingi milioni 100. Elvis Tables Musiba akamuomba katibu muhtasi wake amletee simu. Sikuelewa simu ya nini kwenye kuchangisha fedha. Nilitegemea tungeshirikiana kuandika barua na "proposals" za kuchangisha fedha. Lakini haikuwa hivyo. Simu ilipoletwa akaanza kazi. Alikuwa anatuuliza mnataka kampuni gani ituchangie fedha. Kwa hiyo kazi yetu ikawa ni kutaja majina ya makampuni na yeye anapiga simu. Nilishangaa kuona Elvis Tables Musiba hahitaji tumpe namba za simu. Alinyanyua simu na kupiga kila tulipotaja kampuni. Na alipopiga hakuongea na katibu muhtasi au mkurugenzi wa fedha. Aliongea na CEO, Director General au Mwenyekiti wa "board". Namba alizipata wapi? sijui. Lakini ndani ya saa moja tulikuwa na shilingi milioni 60.

Nikagundiua huyu si mtu wa mchezo. Ana "connections" za ajabu. Nikamuuliza hebu niambie haya mambo unayafanyafanyaje mbona kwangu mageni? Akasema "reciprocate". Hili ni neno la kiingereza linalomaanisha "rudisha wema'. Elvis Tables Musiba aliwasaidia wengi kufika pale walipo ikiwa ni pamoja na CEOs. Kumbuka amekuwa Mwenyekiti wa "boards" za kampuni nyingi. Wengi wa hawa CEOs ameshiriki kuwafanyia usahili kwa wao kuwa pale. Ndio maana haikumchukua muda kupata milioni 60. Alikuwa akiongea na watu ambao ni sehemu ya mchango wake katika maisha ya mafanikio yao. Hii ikanifanya nimdadisi zaidi. Nikamuuliza wewe ulianzaje biashara?

Akasema mtaji wangu wa biashara ulitokana na kuuza vitabu. Vitabu kama NJAMA ndivyo vilivyonitoa. Lakini nilipoanza biashara haikuwa rahisi. Mimi nilikuwa mtanzania wa kwanza "mswahili" kumiliki "Bureau De Change"-anasema Elvis Tables Musiba. Lakini siku moja nikiwa Musoma, nikasikia kwenye redio kwamba biashara yangu iko mikononi mwa serikali. Kidogo nipate kichaa. Lakini sikukata tamaa nikaanza upya. Akasema nyie vijana wa siku hizi mnalalamika mazingira magumu ya biashara. Nawashangaa sana. Tuulize sisi. Haikuwa rahisi kama mnavyofikiria. Kutoka kwa Elvis Tables Musiba nikajifunza yafuatayo;

      I.          Biashara ni mahusiano na watu. Elvis Tables Musiba kutumia saa moja kupata milioni 60 sio mchezo. Aliwekeza kwa watu. Leo hii kutafuta Tsh. 10,000/= ya luku ukikwama usiku wa manane na hauna salio kwenye simu ni shughuli pevu. Unaweza ukapiga namba zote kwenye simu yako usipate hata shilingi moja. Lakini Elvis Tables Musiba alitumia saa moja tu kupata shilingi milioni 60. Ina maana kila dakila alipata shilingi milioni 1.

    II.          Kipaji chako ndio mtaji wako. Badala ya kulalamika huna mtaji, angalia una kipaji gani? Elvis Tables Musiba alikuwa na kipaji cha kuandika hadithi. Ndicho kilichompa mtaji wa kuanzisha biashara. Eric James Shigongo aliwahi kuniambia pia, kwamba kipaji chake cha kuandika hadithi ndicho kilichomsaidia kuanzisha kampuni ya magazeti pendwa na kudumu mpaka leo (Global Publishers). Mifano ni mingi. Bila mpira Mbwana Samata angekuwa wapi? Bila mpira George Weah angekuwa Rais wa Liberia? badala ya kulalamika anza na kipaji chako? Mimi nilianza kwa kuandaa makongamano. Unaweza ukawa unaandaa harusi vizuri kila mtu anashangaa. Lakini bado unafikiri hicho siyo kipaji. Unafikiri kipaji ni "kuimba" tu! Mwenzako makongamano yalinipeleka mpaka Ikulu, yakanipa na mtaji wa kuanza.

  III.          Usikate tamaa. Elvis Tables Musiba anasema amefilisika mara nyingi katika maisha yake lakini alipambana akarudi tena kwenye mstari. Hakujinyonga. Baadhi ya biashara zake zilikwama. Lakini hakukata tamaa wala hakujenga chuki na watu. Kifupi, hakutafuta mchawi. Alianza upya na kusonga mbele. Alishirikiana na watu katika sekta binafsi na serikalini. Hiyo ndiyo roho ya "ujasiri wa mali" au "spirit" ya ujasiriamali au "entrepreneurship". Ni mlolongo wa kushindwa na kushinda, kushindwa na kushinda mpaka kieleweke.

3.     Dr. Reginald Abraham Mengi, Mwenyekiti Mwanzilishi wa IPP Group na Mwenyekiti wa zamani wa CTI na TPSF

Dr. Reginald Abraham Mengi alinishirikisha mwanzoni kabisa wakati akianza kuandika kitabu chake cha "I Can, I Must, I Will". Nakumbuka alinipigia simu akasema njoo ofisini. Akaniambia nataka uwe sehemu ya team itakayonisaidia kukamilisha hili zoezi. Akaniomba nimtafutie vijana wengine wa kushirikliana na Prof. Msamali Nangoli, mwanazuoni wa Uganda aliyekuwa akiishi nchini Kenya, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho "No More Lies About Africa". Prof. Msalami Nangoli alikuwa rafiki mkubwa wa Nelson Mandela, mpigania Uhuru na Rais wa kwanza wa serikali ya kidemokrasia nchini Afrika ya kusini. Akiwa gerezani, Nelson Mandela alikuwa akisoma makala za Prof. Msamali Nangoli, makala ambazo zilipitishwa gerezani kiujanja kama kifungashio cha chapati. Kumbuka akiwa gerezani, Mandela hakuruhusiwa kusoma hata magazeti.

Ili kukamilisha zoezi la kuandika kitabu cha Dr. Reginald Abraham Mengi chini ya uongozi wa Prof. Msamali Nangoli, nilipewa "tapes" za hotuba za Dr. Reginald Abraham Mengi nyingi sana (mabox kwa mabox) ili nizipitie. Pia tuliwahoji watu wengi waliofanya kazi na Dr. Reginald Abraham Mengi. Bahati mbaya sana katikati ya safari ya kumsaidia Dr. Reginald Abraham Mengi kuandika kitabu chake, Prof. Msamali Nangoli akafariki dunia na Dr. Reginald Abraham Mengi akasitisha zoezi kwa muda. Baadaye akapata namna nyingine ya kumalizia kitabu chake kizuri.

Tulipokuwa na Prof. Msamali Nangoli tulimshawishi sana Dr. Reginald Abraham Mengi kubadilisha "title" au jina la kitabu lakini alikataa. Sisi tulipendekeza kitabu chake kiitwe; Dr. Reginald Abraham Mengi-How I became Rich; Financially, Morally, Materially. Lakini hakutaka hata kutusikiliza. Baadaye nilikuja kugundua tulikuwa tunakosea sana kumshawishi abadilishe jina la kitabu cha "I Must, I Can, I Will". Kwanini?

Kwa sababu siku moja nikiwa nyumbani kwake Kinondoni, nilimuuliza. Kwanini "I Must, I Can, I will"?. Akasema kwa sababu maisha ya biashara yana changamoto sana. Akaniuliza Paul, kwani unafikiri changamoto za biashara Tanzania ni zipi. Moyoni nikasema sasa Dr. ananiuliza swali gani "simple" namna hii. Au anataka kupima uwezo wangu wa kufikiri? Nikamwambia kubwa ni 3. Kwanza Mitaji au "Capital", Pili Masoko au "Markets", Tatu Rasilimali Watu au "Human resource". Akasema umekosa. Akasema kwanza Roho Mbaya, Pili Chuki, Tatu Wivu. Nilichoka kichwa. Akasema ili ufanikiwe lazima ukabiliane na hizi changamoto 3 nilizokutajia kisha uunganishe na hizo za mitaji, masoko na rasilimali watu. Ndio maana ya "I Must, I Can, I Will". Lazima udhamirie kutoka moyoni kupambana na changamoto.

Dr. Reginald Abraham Mengi akasema tulipotoka ni mbali kuliko tulipo. Akasema nakumbuka wakati nimeanzisha biashara ya maji ya kunywa, nilienda kwenye maonyesho ya sabasaba kuonyesha biashara mpya ya maji. Akasema watu waliokuwa wakipita kwenye banda langu walikuwa wananishangaa sana. Wanasema "huyu mchaga anapenda sana hela". Mpaka anatuuzia maji? Kweli leo hii nchi hii tumefikia hatua ya kuuziana maji? Dr. Reginald Abraham Mengi akasema kwa hiyo unaweza ukaona "Kilimanjato Pure Drinking Water" imeshamiri ukafikiri ni lelemama. Haikuwa rahisi. Bora hawa ambao wanaanza kuuza maji leo. Sisi tulioanza tulipata shida. Kwa sababu hakuna aliyezoea kuuziwa maji. Lakini Paul ukweli ni kwamba huwezi kushindana na mtu aliyeanza. Aliyekutangulia amekutangulia tu!

Dr. Reginald Abraham Mengi akaendelea kusema zaidi ya hapo kujenga sekta binafsi haikuwa rahisi. Kumbuka historia ya nchi hii toka kipindi cha wakoloni. Toka enzi hizo biashara zilikuwa kwa matabaka. Wa kwanza pale juu ni wazungu, wa pili waarabu na wa tatu wahindi. Sisi wazawa wa "kiswahili" tulikuwa hatufikiriwi kabisa kuwa "matajiri". Kuna wakati nilinunua Mercedez Benz lakini nilikuwa naogopa kuliendesha. Kwa sababu mifumo ya kiuchumi ilikwishakamatwa na matabaka mengine. Kwahiyo unavyoona sekta binafsi imefika hapa ni mapambano kwelikweli. Mswahili kumiliki kiwanda miaka ya sabini na themanini na Mswahili kuwa kiongozi wa sekta binafsi ambayo haina waswahili wengi ulikuwa ni mtihani ambao ilibidi kuushinda. Haikuwa kazi rahisi. Mimi Paul Mashauri nimeona na kusimuliwa mengi pengine nahitaji kitabu kizima kuzungumza ya Dr. Reginald Abraham Mengi. Lakini kuna mafundisho machache nataka niyataje hapa;

      I.          Biashara si lelemama. Changamoto ni nyingi kuliko fursa. Lazima ubadilishe hizo changamoto ziwe fursa ili fursa ziwe nyingi kuliko changamoto. Hii haiwezekani pasipo kuwa na moyo mgumu "a iron heart". Kama unataka uache kazi uanze biashara ukifikiri ni mteremko jifikirie tena na tena na tena. Nakumbuka wakati nimemualika Dr. Reginald Abraham Mengi kuongea na wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam alirudia hilo. Akasema; "safari ya mafanikio ni kama pambano la ngumi. Kuna makonde ya kuyakwepa, kuna makonde ya kuyazuia ambayo yakikupata yanasambaratisha uso wako au kukuua kabisa lakini kuna wakati ambao lazima ujibu mapigo ili ushinde pambano. Mh. Jokate Mwegelo, DC, Kisarawe, kipindi hicho akiwa chuoni, alikuwa "Moderator" katika tukio hilo. Anaweza akayakumbuka maneno haya.

    II.          Usiogope kuanzisha njia pasipo na njia. Usiogope kuwa wa kwanza kufanya jambo ambalo wengine wanasita kufanya. Maana yake ni kwamba "be the pioneer". Dunia tunayoishi iko hapa ilipo sababu ya "pioneers". Christopher Columbus angeogopa kusafiri kutoka Spain pengine America (New Land) ingechelewa sana kutambulika katika uso wa dunia. Hata wewe usiwe mtu wa kusubiri wenzako waanze. "Legends" sio wale wanao "copy na kupaste" Legends ni waanzilishi. Kuanza sio lazima iwe ni kwenye biashara. Hata kwenye familia yako unaweza ukawa wa kwanza kuwa "mbunge".

4.     Mr. Ali Mfuruki, Aliyekuwa Mwenyekiti wa CEO Round Table

TRBN (Tanzania Responsible Business Network) ilipoanza niliombwa na Partner wa KPMG Ketan Patel pamoja na Partner wa Deloitte Joe Eshun niwe "Moderator" katika sherehe za uzinduzi wa TRBN pale Serena Hotel. Tulikuwa na CEOs zaidi ya 300. Mgeni rasmi alikuwa ni Mr. Ali Mfuruki, Mwenyekiti wa CEO Round Table. Baada ya ufunguzi nilikuwa na muda wa kutosha wa kuongea na Mr. Ali Mfuruki. Jambo moja Mr. Ali Mfuruki aliniambia ambalo sitolisahau ni kwamba lazima uwe na msimamo na lazima ukubali kupoteza baadhi ya vitu ikiwa ni pamoja na fedha kusimamia unayoyaamini. Akaniambia nyie vijana sasa hivi ndio mmekuwa mameneja kwenye makampuni na viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali. Sasa wakati mwingine unakutana na kijana kwenye kampuni ambaye amepewa mamlaka, kijana ambaye unaweza kumzaa anataka akuzungushe, akunyanyase ili umpigie magoti. Mimi siwezi. Bora nikose hela kuliko kushusha heshima yangu.

Wapo vijana ambao wanamsikia Mr. Ali Mfuruki leo hii lakini hawajakutana na Mr. Ali Mfuruki na kuzungumza naye ana kwa ana. Sijui umesikia nini juu yake lakini Mr. Ali Mfuruki alikuwa na msimamo wa kipekee. Alikuwa anafikiria vizuri sana sio katika biashara zake tu hata kwa nchi. Ndio maana kifo chake kimetushtua kama Taifa. Unaweza ukawa unafikiria vizuri lakini kwa mambo yako binafsi na familia yako. Hilo ni jambo zuri na ndiyo jambo la pili baada ya kumfikiria Mungu. Lakini unapojiongeza na kufikiria Taifa na watu wengine ndani ya Taifa unakuwa wa tofauti zaidi. Ndivyo alivyokuwa Mr. Ali Mfuruki.

Kuna siku nilikutana naye nikamuuliza Mr. Ali Mfuruki lini unaandika kitabu? Akaniambia nimeanza kuandika. Siku niliposikia ametoa kitabu, nikawahi bookshop Mlimani City kununua. Lakini baada ya kusoma kile kitabu nikagundua nilichofikiria kuwa kitakuwepo kwenye kitabu sicho. Mr. Ali Mfuruki hakuwa ameandika kitabu kuhusu yeye na mke wake na watoto wake. Alikuwa ameandika kitabu kuhusu uchumi wa viwanda. Huyo ndio Mr. Ali Mfuruki. Ndiyo sababu alidumu kama Mwenyekiti wa CEO Round Table kwa miaka mingi. Sio kwamba alipenda kuhodhi madaraka. Alikuwa ana uwezo kichwani. Na vyeo vingi alikuwa anakataa. Na pale alipokubali alijitoa kwa dhati. Amekuwa Mwenyekiti wa "boards" za Mwananchi Communications Ltd, amekuwa kwenye "board" ya Geita Gold Miming (GGM), Mwenyekiti wa "board" ya Vodacom nk. Waulize waliofanya kazi naye. Kile kilikuwa kichwa kingine.

Wakati fulani nilialikwa katika uzinduzi wa "Private Equity Fund" moja pale Golden Tulip Hotel. Alikuwepo Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Mh. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waheshimiwa mawaziri na wafanya biashara. Mr. Ali Mfuruki alikuwa miongoni mwa waalikwa pia. Siku ile Mr. Ali Mfuruki aliongea kitu kikubwa sana. Akasema, wakati Marekani inataka kwenda mwezini miaka ya 60. Rais wa nchi hiyo J.F. Keneddy alitangaza kwamba Mmarekani yoyote atakayekuja na wazo au "idea" au "ubunifu" au "teknolojia" ambayo itaisaidia Taifa la Marekani kufika mwezini au kufika hatua moja mbele katika ndoto ya nchi kwenda mwezini, serikali ya Marekani italipa fedha kununua hilo wazo au huo ubunifu. Mr. Ali Mfuruki akasema; ili sisi kama Taifa tuweze kwenda mbele lazima kuwe na mbinu za kujenga "uhitaji" au "demand" ya ugunduzi na ubunifu "Creativity and innovation" . Akasema "kufikiria" ni kazi. Kugundua kitu ni gharama. Lazima ufanye "research" au "utafiti". Tukitaka watu wetu wawe wabunifu lazima tutengeneze mbinu za kumfikirisha mtu akijua kabisa kuwa nguvu zake hazitoenda bure.

Mr. Ali Mfuruki alikuwa haongei "nadharia". Sijawahi kumsikia akiongea "pumba". Kwa historia yake yeye ni mhandisi au "engineer" kwa lugha ya kiingereza. Mr. Ali Mfuruki Alipotoka nchini Ujerumani aliposomea, kuja nyumbani Tanzania kufanya biashara, aliona kuna fursa, kuna "demand" au "uhitaji" wa bidhaa za teknolojia hasa kompyuta. Kipindi hiki nchi ilikuwa imefunguka na serikali pamoja na makampuni binafsi yalikuwa yanabadilisha teknolojia kutoka katika mfumo wa kizamani wa "fax" na "typewriters" kuja kwenye matumizi ya kompyuta. Ndivyo kampuni yake ya Infotech Technologies Ilivyoanza. Huwezi kuzungumzia Teknolojia Tanzania pasipo kumzungumzia Mr. Ali Mfuruki ingawa amekuwa na biashara nyingi zaidi ya hiyo. Yeye ni baba katika eneo hili la TEHAMA hapa Tanzania pamoja na kwamba unapozungumzia ujio wa WoolWorth unamzungumzia Mr. Ali Mfuruki na hata unapozungumzia ujio wa Zuku unamzungumzia Mr. Ali Mfuruki. Nini cha kujifunza hapa;

      I.          Tunaishi katika dunia ya ubepari au "capitalism". Dunia ya "ubepari" na dunia ya ujamaa au "socialism" ni dunia 2 tofauti. Katika dunia ya ubepari mtu anaweza akakudhalilisha kwa sababu amekupa fursa. Mtu anaweza akataka umuabudu na umpigie magoti kwa sababu anakupa biashara. Mtu anaweza akakuvunjia heshima mbela ya mke na watoto wako kwa sababu bila yeye huwezi kupata mshahara. Haya ndiyo mambo ambayo Mr. Ali Mfuruki aliniambia hayataki. Akasema bora niwe "broke" au "masikini" kuliko kudhaliliswa. Alikuwa na msimamo.

    II.          Vijana wengi wanatamani kuheshimiwa kama Mr. Ali Mfuruki. Lakini hawajui kuwa heshima haiji kwenye kikombe cha chai. Inajengwa kwa jasho kubwa. Mimi Paul Mashauri ambaye nimekaa na hawa watu najua. Mimi Paul Mashauri ambaye nimetumika sana kwenye sekta binafsi nijaua. Ni kazi ngumu na inataka moyo. Kumbuka Mr. Ali Mfuruki ni mfanyabiashara. Ana biashara zinazomuangalia yeye. Na bado aangalie ya nchi. Sio jambo dogo. Kumbuka akifanya hivyo waziri ni sawa kwa sababu mwisho wa mwezi analipwa mshahara. Ni sehemu ya "job description". Lakini unapokuwa Mwenyekiti wa hizi taasisi za sekta binafsi unatumia akili zako na nguzu zako kama msaada na mchango kwa Taifa. Ingawa sina uhakika kama ukifilisika unapewa tena mtaji na Taifa. Ndio maana nasema inataka moyo. Ni vijana wangapi wako tayari kufanya hivyo? Kuacha biashara yako na watoto wako kuhangaikia ya wengine?

  III.          Mr. Ali Mfuruki alikuwa anafikiri vizuri "thinker" kwa sababu alikuwa anatumia muda mrefu sana kukutana na watu wa haiba tofauti, kusoma, kusafiri kupata "exposure" nk. Hakuna mtu alikuwa anamlipia tiketi ya ndege kusafiri. Alikuwa anajilipia mwenyewe. Leo unataka kuwa kama Mr. Ali Mfuruki unashinda instagram unasoma udaku. Hautaki kwenda kwenye kongamano lolote zaidi ya matamasha ya muziki na comedy. Kila tasnia ina utamaduni wake. Ukitaka kuketi katikati ya wakuu lazima ufikirie kama wakuu. Mr. Ali Mfuruki aliitwa na wakuu, alikaa meza moja na wakuu akiwemo Barack Obama, Rais Mstaafu wa Marekani sio kwa sababu alikuwa "handsome" mwenye "six packs" tumboni kuliko watanzania wote. La hasha! Alikuwa na madini adimu kichwani.

5.     Ruge Mutahaba, Aliyekuwa Mkurugenzi au "Director" wa programs, Clouds Media Group

Niliposikia amefariki, nilisikitika sana. Kwa sababu miezi michache iliyopita kabla ya taarifa hizo nilimpigia simu. Nikamwambia kaka Ruge kuna kongamano la vijana na wazazi tunaandaa naomba uje uzungumze hasa na vijana. Akajibu akasema "count me in". Lakini miezi kadhaa nyuma, Ruge mwenyewe alinipigia simu. Akasema Paul wewe na mimi kama "speakers" lazima tufanye mambo ya kusaidia nchi. Akaniambia hebu andika "andiko" au "proposal" ya kusaidia Taifa letu kwa kutumia "speakers" kuhamasisha fikra mbadala hasa katika mambo ya msingi ya kitaifa. Nilikesha usiku ule nikaandika ile "proposal" na nikamtumia Ruge kwa email. Ile "propoal" niliipa jina la "Speakers Without Boarders".

Wengi walimfahamu Ruge Mutahaba kwenye "media" na "muziki" lakini Ruge Mutahaba alikuwa ni zaidi ya media na muziki. Ndio sababu alipofariki hata Rais wa nchi alitoa neno. Uwezo wa Ruge Mutahaba ulikuwa hauna shaka. Ubishi wake kwa kile alichokiamini ulikuwa si wa kitoto. Na utayari wake kujitoa kwa ajili ya wengine hauelezeki. Siweki chumvi na mimi sio mnafiki wala sisemi haya yote kwa sababu hayupo tena duniani. Niliyasema haya hata alipokuwa hai. 

Niliyasema ya Mr. Ali Mfuruki wiki iliyopita ambayo ni wiki moja kabla hajafariki. Sio wote wana moyo wa kusema nani aliwasaidia katika maisha yao lakini mimi nasema kwa sababu duniani hakuna mtu anayetoka bila msaada wa mtu mwingine. Hakuna kitu kama "self-made". Kusaidiwa sio lazima iwe pesa .Hata mwalimu wa shule ya msingi alikusaidia kujua kusoma na kuandika. Leo unasemaje kuwa wewe ni "self-made millionaire"? Humkumbuki hata mkeo au mumeo aliyekutia moyo ulipokata tamaa?

Ruge Mutahaba alinisaidia sana mimi na vijana wengine wengi. Yeye ndiye aliyenitambulisha kwa Azim Jamal aliye kuja kuwa rafiki yangu mkubwa katika "motivational speaking". Huyu ni mnenaji au "speaker", mwandishi wa vitabu au "author", mtaalam wa menejimenti au "consultant" na mfanyabiashara aliyebobea. Azim Jamal amefanya kazi na kuandika vitabu pamoja na wataalam na wanenaji "speakers" wakubwa duniani kama Brian Tracy. 

Kumlipa Azim Jamal kuzungumza kwenye tukio lako sio chini ya dola za Kimarekani milioni 10 au fedha za kitanzania zaidi ya shilingi milioni 20 ndani ya siku moja. Lakini kwa sababu ya urafiki na heshima ya Ruge Mutahaba, Azim Jamal alikuja kuzungumza kwenye tukio nililoandaa bila kulipwa hata shilingi moja. Baada ya hapo tulifanya kazi nyingi sana na Azim Jamal.

Pili wakati tunaanzisha gazeti la Familia, yeye ndiye aliyenipa matangazo ya bure. Alisema wewe unafanya kazi kubwa sana kuhamasisha vijana. Hakuna anayekulipa kwa kujitolea kwako. Malipo yako yatakuwa matangazo nitakayokupa Clouds FM. Kwa moyo ulionao ukitoka wewe, wengi zaidi watatoka. Ruge Mutahaba alilipa gharama ya kazi yangu kwa vijana. Si hayo tu, yeye pamoja na Joseph Kusaga ndio walionipa studio za Clouds TV kutengeneza sinema yangu iitwayo "Maisha Ni Siasa". 

Angalia sinema hii yote Youtube. Sio mimi tu, wako wengi aliowasaidia. Hata serikali inatambua nini Ruge Mutahaba alifanya katika nchi hii. Uzoefu wangu wa Ruge Mutahaba tukiwa wajumbe wa TRA Stakeholders Forum ulinidhihirishia uwezo wake wa kuangalia mambo kwa jicho la tatu. Ndio sababu alikuwa mbunifu sana. Kila tulipokuwa na kikao, Ruge Mutahaba hakuwa wa kwanza kuongea. Lakini alipopata nafasi ya kuongea, aliipindua pindua mada na wote tukaiona hoja husika kwa namna ambayo hatukuiona hapo kabla.

Kila nikimkumbuka Ruge Mutahaba nakumbuka mmoja kati ya vijana ambao walijiongeza. Ungeniuliza ni akina nani wanafanya sana kazi bila kuchoka ningekuambia ni Ruge Mutahaba. Binafsi sijui alikuwa anapumzika saa ngapi. Unakutana na kijana anasema anataka kuwa kama Ruge Mutahaba na bado analala saa 2 usiku na anaamka saa 2 asubuhi. Unataka kuwa kama Ruge yupi? Sijaona mimi mtu anafanya vitu vikubwa vya kitaifa na analala usingizi wa pono. Uliza wasaidizi wa Rais kama wanalala? Kama unajua huwezi kufanya kazi kwa bidii kubali kuwa wa kawaida. Usifikiri nazungumzia "utajiri". Hilo ni suala lingine.

 Unaweza usiwe tajiri lakini bado ukawa si wa kawaida. Akina Dr. Martin Luther King Jr. na Nelson Mandela hawakuwa matajiri lakini pia hawakuwa wa kawaida. Lazima utofautishe kati ya kuwa "rich" au "tajiri" na kuwa "great". Hapa sizungumzii utajiri nazungumzia "greatness". Hata mwizi anaweka kuwa "tajiri" lakini inahitaji "akili nzuri", "kujitoa kwa wengine" na "kujituma" ili uwe "great" Vitu vinavyobadilisha jamii havihitaji mtu mzembe. Kama kusoma tu hii makala mpaka hapa umeshachoka unatamani iishe utaweza kuwa kama Ruge Mutahaba? Kuna mambo ya msingi ya kujifunza kutoka kwa Ruge Mutahaba;

      I.          Ubishi. Hakuna kitu kinakuja kirahisi. Mafanikio sio muujiza, yanafanyiwa kazi. Usifikiri Ruge Mutahaba alifika pale alipofika sababu ya "Clouds" kama media. Hatukatai ukweli kwamba alikuwa ni mmoja wa watu walioijenga Clouds Media Group. Kwanza, ulikuwa ukisikia Clouds FM iko hewani, sura mbili zinakuja kichwani kwako; Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga. Hata isingekuwa "media" Ruge Mutahaba angefanya vitu vikubwa tu kwa sababu alikuwa ni "mbishi" asiyekubali kushindwa. Miaka 3 iliyopita nilimualika Ruge Mutahaba katika kongamano la Vijana lililoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji (NEEC) pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO) pale Serena Hotel. Kongamano lilikuwa chini ya mradi wa kutoa mitaji kwa mawazo bora ya biashara kwa vijana "Ajira Yangu" Project ambayo niliisimamia.

    II.          Alipopewa nafasi ya kuzungumza, Ruge Mutahaba akasema "ukija kwangu na wazo au "idea" yako nakurudisha mara 3 au mara 4. Sio kwa sababu wazo lako ni baya. Nataka nione kama kweli wewe ni mbishi na uko tayari kupambana mpaka wazo lako lipate maisha. Vijana wa leo hawako hivyo. Wanataka mambo ya chapchap kama mabando ya internet. Hawana uthubutu. Wanaamini kwenye michongo na kushikwa mkono. Wanakata tamaa mapema. Hata wakija kwako uwe "mentor" wao wanakuja "kifursa zaidi". Wanataka uwe "mentor" wao na hapohapo uwape "hela". Hiyo sio "mentorship" hiyo ni "sponsorship". Sasa hatujui unataka nini? Unataka "mentorship" au "sponsorship"?Hawajui kuwa hata akina Ruge Mutahaba walipitia vikwazo lakini walikuwa wabishi.

  III.          Uwezo wa kufanya lolote unalolitaka. Nilisema hapo mwanzo kwamba wengi wanamjua Ruge Mutahaba kwa sababu ya "media", "muziki" na "matamasha". Ruge Mutahaba alikuwa zaidi ya hapo. Ruge Mutahaba alikuwa pia anandaa sinema. Nikiwa chuo kikuu Ruge Mutahaba alirekodi sinema inaitwa "Kelele". Yeye mwenyewe binafsi alikuwa nyuma ya kamera kuhakikisha sinema inarekodiwa vizuri. Ingawa sikumbuki kama aliwahi kuitoa ile sinema lakini nilichojifunza ni kwamba alijua anaweza kufanya kitu zaidi ya kimoja.

 Kuna mikakati mingi sana na miradi mikubwa ya kitaifa mbayo Ruge Mutahaba alikuwa nyuma yake ingawa hakuonekana mstari wa mbele. Huyo ndiyo Ruge Mutahaba niliyemfahamu mimi. Leo hii unatamani siku moja upewe heshima aliyopewa Ruge Mutahaba lakini hujiulizi nini kitu cha tofauti unafanya? Zaidi ya kutoka bwenini, kwenda darasani kisha kwenda bwaloni kula ubwabwa nini kingine unafanya? Zaidi ya kutoka kazini na kwenda baa au kwenye harusi kula pilau, nini kingine unafanya?Unawezaje kuwa kama Ruge au zaidi ya Ruge kwa maisha ya pembe tatu?Unawezaje kufikia ndoto zako kwa maisha ya pembe tatu? Hata kama umeajiriwa. Usiku unafanya nini?

Tanzania imepoteza watu muhimu sana katika muda mfupi sana. Niliyoyataja hapa kwa hawa "generals" ni machache sana ukilinganisha na niliyoyafahamu na nisiyoyafahamu. Hawa watu walitumia vyema uwepo wao hapa duniani na uwepo wao katika hii nchi kuleta utofauti. Ni "generals" walioondoka lakini nchi bado ipo. Pamoja na utofauti wao, hawa wote wanasifa zinazofanana. Pamoja na mapungufu yao wote hawa wana faida zinazofanana.

1. Waliwekeza katika maarifa 2. Waliwekeza katika watu 3. Walitumia karama, vipaji na elimu zao kuleta utofauti na kulitumikia Taifa 4. Hawakuwa wepesi kukata tamaa hata walipopitia magumu katika ngazi za familia zao, maisha yao binafsi, biashara zao na kazi za kitaifa 5. Wameacha alama katika nchi hii, alama ambayo itaendelea kuishi ingawa wao hatunao tena. Amani ya bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nao, familia zao, ndugu zao, marafiki zao na watanzania wote kwa ujumla.  
Makala hii imeandikwa na Paul R.K Mashauri@hakimiliki 2019. Hairuhusiwi kuchapisha Makala hii au sehemu ya Makala hii pasipo idhini ya mwandishi. Wasiliana na mwandishi kupitia ceo@masterclassworldwide.co.tz

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527