CCM YAWEKA MIKAKATI KUMNG'OA MSIGWA JIMBO LA IRINGA MJINI


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally, akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Iringa, amewahakikishia wanachama, mashabiki na wakereketwa wa CCM kuwa Chama hakipo tayari kupoteza jimbo la Iringa Mjini kama ilivyofanyika miaka michache nyuma.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa kamati za siasa za wilaya ya Kilolo, Iringa Mjini na Iringa Vijini mara baada ya kupokelewa akitokea Mkoani Dodoma.

“Ujumbe ninao utoa kwa vyama vya upinzani leo tarehe 17 Desemba, 2019 ni kuwa, nataka jimbo la Iringa mjini na Manispaa yake lirudi CCM, na Mkoa wa Iringa umekuwa ni ngome ya CCM miaka yote, hapa mjini yalifanyika makosa ambayo ndani ya uongozi huu hayatojirudia tena.”

Aidha Katibu Mkuu ameongeza kuwa, Jimbo hilo lilipotea kutokana na migawanyiko ndani ya CCM, na awamu hii, jimbo na manispaa yake inarudi CCM na Chama hakitarajii kufanya makosa tena.

Katika hatua nyingine, Dkt. Bashiru ameendeleea kuwaasa wanaCCM kuwa, heshima wanayopatiwa viongozi, ni heshima kwa Chama, ambapo ndani ya CCM hakuna mtu maarufu wala kiongozi maarufu kuliko chama, nje ya Chama, hakuna mtu maarufu hivyo ni lazima viongozi na wanachama wajue wanapata heshima kwa sababu ya Chama na ni lazima tukilinde ili kiendelee kubaki na heshima wakati wote.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kueleza msimamo wa CCM katika uongozi, ambapo ni mtu mmoja kofia moja na kiongozi yeyote hana sababu ya kujiuzulu nafasi aliyonayo kabla hajapata nafasi aliyoiomba, hivyo ameshauri nchi nzima wale waliojiuzulu nafasi zao kwa lengo la kugombea serikali za mitaa na hawakufanikiwa kuchaguliwa, warudi kwenye nafasi zao kwa kuwa wengi hawakuwa na sababu za msingi.

Katibu Mkuu yupo Mkoani Iringa kwa siku mbili ambapo kesho atakuwa mgeni maalum katika uzinduzi wa chuo cha Mafunzo cha CCM Ihemi kitakachofunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara Ndg. Philip Japhet Mangula.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post