WAZIRI KALEMANI ATEUA WAJUMBE WA BODI TANESCO

WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameteua Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yenye wajumbe wanane.


Dkt. Kalemani amefanya uteuzi Novemba 13, 2019, unatokana na Rais John Magufuli kumteua Dkt. Alexander Kyaruzi kuwa Mwenyekiti wa Bodi kwa kipindi kingine cha pili.

Rais Magufuli alimteua Dkt. Kyaruzi Novemba 9, mwaka huu baada ya kuwa ameshika wadhifa huo kuanzia Mei 2016 hadi Mei 2019.

Dkt. Kalemani alisema wajumbe hao wapya watakaa madarakani kuanzia Novemba 13, 2019 hadi Novemba 12, 2022.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Balozi Dk James Nzagi (alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO iliyomaliza muda wake) na Dkt. John Kihamba (Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Saam - DUCE).

Wengine ni Dk Lugano Wilson (Mkurugenzi wa Maendeleo ya Uhandisi na Mkuu wa Teknolojia za Nishati - TIRDO), John Kulwa (Mkuu wa Idara ya Ukaguzi Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi - MUHAS) na Denis Munumbu (Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU).

Wengine ni Dk Gemma Modu (Mkurugenzi NACTE), Mathew Kirama (Mkurugenzi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Gilay Shamika (Mjumbe katika bodi iliyopita).

Dkt. Kalemani alimpongeza Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua tena Dkt. Alexander Kyaruzi kuisimamia Bodi hiyo.

Alimtaka Mwenyekiti huyo kulitumikia Shirika kwa Kasi, weledi na nidhamu ili kuwahudumia watanzania kwa kuondoa kero ndogo na kuifanya heshima ya Watanzania kwa TANESCO iendelee.

"Ni matumaini yetu mtakuja na ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya katika kutekeleza azma ya Hapa Kazi Tu ili kulipa nguvu Shirika letu," alisema Dkt. Kalemani.

Kwa wajumbe wote, aliwataka wachape kazi ili kuhakikisha wadau wa Tanesco wanafaidi huduma nzuri na kuhakikisha Umeme unawafikia watanzania wote.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Dk Kyaruzi alimshukuru Rais Magufuli kwa heshima kubwa kwake kwa kumteua tena kulisimamia shirika hilo.

Alisema TANESCO miradi mingi ya kimkakati ukiwamo Mradi wa Kufua Umeme wa Maporomoko ya Maji wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 na wa Rusumo mkoani Kagera.

Alisema miradi hiyo na mingine wataisimamia kikamilifu kwa kuweka mikono yao humo kwa kufuata miongozo mbalimbali wanayopewa na viongozi wao.

Miongoni mwa waliohudhuria ni kikao hicho ni, Naibu Waziri Nishati Mhe. Subira Mgalu, Katibu Mkuu Nishati Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mhandisi Leonard Masanja Kamishina wa Umeme na Nishati Jadilifu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) Dkt. Alexander Kyaruzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt.Tito Mwinuka na Viongozi Wandamizi wa Wizara ya Nishati.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527