WAPANGAJI WA NYUMBA ZA NHC KUHAKIKIWA UPYA


Waziri wa Ardhi Mhe.William Lukuvi ametoa miezi 4 NHC kuhakiki wapangaji wa nyumba pamoja na majengo yao na kisha kuanzisha nyaraka za Kielektroniki zitakazosaidia kubaini wajanja wanaopangisha na kujimilikisha nyumba za shirika hilo kinyume cha sheria.



Lukuvi, alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam baada ya juzi kutembelea miradi ya shirika na kutaka ifikapo Machi 30, mwakani, uhakiki huo uwe umekamilika.

“Ninajua kuna baadhi ya wapangaji wameanzisha vishirika vya nyumba ndani yenu, kuna watu wana nyumba mbili au tatu kwa ujanja wao na wao wanakodisha. Tutawaondoa wapangaji hewa na tutawatambua wamiliki hewa wa nyumba zilizotaifishwa.

“Kuna watu wakihama kwenye nyumba wanaziuza kwa gharama kubwa wanachukua fedha juu ya mgongo wa shirika hili kwa sababu inaelekea hatuna utunzaji wa kisasa wa takwimu za wapangaji na nyumba.”

Pia, alilitaka shirika hilo liingie kwenye utaratibu wa kidijitali kwa kuanzisha nyaraka za kieletroniki ili kutunza kumbukumbu za wapangaji.

“Taarifa hizi ziingie kwenye mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa (Nida), wapangaji wote lazima wafanyiwe uhakiki taarifa zao zifanane na taarifa za Nida.

“Kila mpangaji anapohamia kwenye nyumba tumjue anafanya kazi wapi, jina lake kamili kama alivyojiandikisha Nida.”

Alisema anawajua baadhi ya watu wanaomiliki zaidi ya nyumba moja kwa majina tofauti na wengine wanazitumia kuzikodisha huku wakiwa kwenye majengo mengine.

“Wote watambuliwe, najua kuna vishoka ambao wanaowatumia kuzikodisha, mfanye uhakiki upya wa kielektroniki. Wakati wa uhakiki hakikisheni maofisa na mameneja wa Mkoa wa Dar es Salaam wanaondolewa na kuwekwa watu wengine,” alisema.

Waziri Lukuvi aliwaeleza wananchi kuwa nyumba za shirika hazitolewi kwa familia kama urithi baada ya aliyepangishwa kufariki, bali waliobaki hutakiwa kwenda NHC kwa ajili ya upangaji upya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527