WAFANYABIASHARA ARUSHA WAPEWA SIKU MOJA KUHAMISHIA SHUGHULI ZAO NDANI YA SOKO

Na Tito Mselem Arusha,

Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa siku moja kwa Wafanyabiashara wote wa Madini Mkoani Arusha kuhamishia shughuli zao ndani ya Soko na watakao bainika kununua madini nje ya Soko watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni zao na kufikishwa Mahakamani. 

Hatua hiyo inafuatia ziara ya kushtukiza ya Waziri Biteko aliyoifanya Sokoni hapo Novemba 13, 2019 na kubaini changamoto za wanunuzi Wakubwa wa Madini kutolitumia Soko hilo na badala yake wameendelea kununua Madini nje ya Soko.

Katika zira yake hiyo, Waziri Biteko ameambatana na viongozi mbalimbaliwa Serikali pamoja na Wizara ya Madini akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Mkoa wa Arusha Jonathan Shanna na wengine.

Pia, Waziri Biteko amemtaka Mkandarasi anayeendelea na ujenzi katika Soko hilo ahakikishe anamalizia haraka ujenzi huo huku wafanyabiashara wakiwa wanaendelea na shughuli zao katika Soko hilo.   

Aidha, Waziri Biteko amemuagiza Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula kumuondoa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Robert Erick kwa kushindwa kusimamia ipasavyo shughuli za Madini Mkoani humo.

Afisa Madini huyo anadaiwa kuwaachia wafanyabiashara wakubwa wa Madini Mkoani Arusha kufanya biashara ya Madini maofisini mwao tofauti na maelekezo ya Serikali iliyowataka wafanye biashara hiyo kwenye Masoko ya Madini ambapo ofisi nne tu ndizo zilikuwa wazi wakati Soko hilo lina ofisi za wafanyabiashara wakubwa 40 lakini kwa zaidi ya miezi minne hawajahamia katika ofisi hizo.

Alisema jukumu hilo la kusimamia kufanya biashara ndani ya Soko hilo na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wenye madini majumbani mwao ni jukumu la Afisa Madini, lakini kazi hiyo kwa sasa inafanywa na Waziri hatua ambayo haikubaliki kabisa, wakati wa kulindana umepitwa na wakati sio kwa Serikali hii iliyopo madarakani.

Waziri Biteko alisema kuwa, biashara ya Madini ya Tanzanite Mkoani Arusha imeshuka kwa asilimia kubwa na wanaofanya biashara hiyo wanajulikana  lakini hawachukuliwi hatua  na kwamba ofisi yake haiko tayari kuona ubadhilifu wa aina hiyo.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Biteko amesema kuwa haoni sababu za msingi za wafanyabiashara wakubwa wa Madini Mkoani Arusha kushindwa kufanya biashara katika Soko la Madini lililoandaliwa na Serikali na badala yake wafanyabiashara hao wanafanya biashara katika ofisi zao.

Amewaeleza wafanyabiashara Wakubwa na Wadogo wa Madini Mkoani Arusha kuwa haitaji kupigiwa makofi kwani yeye anasimamia kanuni na sheria namba 20 ya Madini inayosema kuwa kila mfanyabiashara wa Madini awe Mdogo ama Mkubwa anapaswa kufanya biashara ndani ya Soko la Madini na sio vinginevyo.

Ameongeza kuwa, Wafanyabiashara wakubwa waliomba muda wa mwezi mmoja katika kufanya biashara ndani ya Soko hilo na Wizara iliongeza muda huo waliohitaji lakini hadi sasa ni zaidi ya miezi minne hakuna mfanyabiashara mkubwa aliyekuwa akifanya bishara katika Soko hilo na badala yake wanafanya biashara katika ofisi zao na wanamiliki kilo nyingi za madini kinyume cha utaratibu.

Waziri amesema anazo taarifa za uhakika baadhi ya wafanyabiashara wakubwa 97 wana ofisi za madini Arusha na Nairobi na wanafanya ujanja ujanja ili wafanye biashara hiyo kwa njia haramu na kuikosesha Serikali mapato hilo halikubaliki watachukuliwa hatua kali ikiwemo kufilisiwa mali zao na kufikishwa Mahakamani.

Akizungumzia suala la wafanyabishara Wadogo wa Madini amesema ofisi yake ina idadi ya wafanyabishara wenye leseni  263 lakini wanaofanya biashara hiyo mtaani ni zaidi ya watu 1,300 hali inaonesha wazi kuwa  zaidi ya wafanyabiashara 1037 wanafanya biashara bila ya kuwa na leseni na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha analijuwa hilo lakini ameshindwa kusimamia majukumu yake ya kazi.

Pamoja na mambo mengine Waziri Biteko amesisitiza uaminifu katika sekta ya madini.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527