RAIS MAGUFULI AFUNGUKA MAZITO KUHUSU UHURU WA KISIASA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania katika mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic uliofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre(JNICC)

Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) amesema, uhuru wa kisiasa hauna maana kama nchi za Afrika zitaendelea kuwa tegemezi kiuchumi.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Novemba 2019, wakati akifungua Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na NORDIC, jijini Dar es Salaam.

“Viongozi wengi wa Afrika tumetambua kuwa, mustakabali wa Bara letu uko mikononi mwetu, na kwamba uhuru wa kisiasa hauwezi kuwa wa maana sana, endapo mataifa yetu yataendelea kuwa tegemezi kiuchumi,” amesema Rais Magufuli.

Na kwamba, mataifa ya Afrika hayawezi kuwa Huru wa kujiamulia masuala yake, iwapo yataendelea kuwa ombaomba. Na kuwa, viongozi wa Bara hilo jukumu lao ni kutafuta ukombozi wa kiuchumi.

“Hatuwezi kuwa na Uhuru wa kujiamulia mambo yetu wenyewe, endapo mataifa yetu yataendelea kuwa ombaomba. Kutafuta ukombozi wa kiuchumi ndio jukumu la viongozi wa Afrika. Hata Mwalimu Julius Nyerere alisema, ukombozi wa Afrika ni kujikomboa kiuchumi,” amesema Rais Magufuli.

Pia, amesema ushirikiano wa kutoa na kupokea misaada, hauhitajiki kwa sasa, kwani sio endelevu.

“Pamoja na uhusiano mzuri na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye ushirikiano, bado tuna fursa ya kukuza ushirikiano wetu ili kuleta manufaa kwa pande zote mbili.

“Na suala hili ni muhimu kwasababu, kwa muda mrefu ushirikiano wetu umejikita zaidi kwenye kutoa na kupokea misaada, ushirikiano wa aina hii sio endelevu na wala hauhitajiki katika mazingira ya sasa, “ amesema Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa Tanzania amependekeza nchi za Afrika kubadilisha ushirikiano, kutoka kwenye ushirikiano wa kupokea misaada, kwenda kwenye ushirikiano wa kiuchumi.

“Ni lazima tubadilishe muelekeo na kuingia kwenye uhusiano wa kisasa baina ya mataifa, ambao unajikita kwenye uchumi kupitia biashara na uwekezaji. Diplomasia ya uchumi ndio iwe kwenye ushirikiano kwa mataifa yetu,” ameeleza Rais Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527