KAMATI ZA RUFAA UCHAGUZI KUMALIZA KAZI LEO..JAFO ASEMA 'UKITEULIWA JINA LAKO LITABAKI KWENYE KARATASI YA KUPIGIA KURA HATA KAMA UMEJIENGUA''


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amesema kamati za rufaa za uchaguzi wa serikali za mitaa zitakamilisha kazi yake leo, huku akisisitiza kuwa jina la mgombea likiteuliwa litabaki kwenye katarasi za kupigia kura hata kama amejiengua kushiriki.

Aidha, amesema zaidi ya rufaa 13,500 zimewasilishwa na vyama vyote vya siasa kwenye kamati hizo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dodoma, Jafo amesema vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo vilipeleka rufaa kwenye kamati za maeneo yao na tayari zingine zimeshatolewa maamuzi.

Aidha amesema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo mtu akiteuliwa jina lake linabaki kwenye karatasi za kupigia kura.

“Jina lako limeteuliwa wewe ukasema labda mimi sishiriki jina lako litakuwa kwenye ‘ballot paper’ kwa mujibu wa kanuni zetu, sasa wewe kupanga ni kuchagua,”amesema.

Amebainisha “Kesho tutapata sura halisi ya mchakato mzima wa uchaguzi haya mapingamizi yamewasilishwa kwenye kamati za rufaa za maeneo husika ambapo mwisho wa kupitia rufaa hizo ni leo na zinafanya kazi kwa mujibu wa ibara ya 23 ya kanuni zetu.”

Ameongeza kuwa “Nilishasema malalamiko yote yapelekwe kamati za rufaa kwa kuwa zinafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na hizi kamati hazifungwi na mtu, nashukuru baadhi ya vyama vimewasilisha na kazi inaendelea ya kupitia rufaa hizo ikiwa leo ni mwisho.”

“Kesho tutatoa taarifa ya rufaa zilizopita na watu walioteuliwa kushiriki uchaguzi huo, tunaendelea vizuri tunatarajia leo jioni zitakamilisha kazi kamati za rufaa na zinafanyia kazi rufaa zote kwa kuwa ziliwasilishwa na wagombea, na watatoa matokeo kwa vyama vyote lakini kamati ya rufaa itakuwa imetimiza wajibu wake,”amesema.
Via Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527